Wakulima walianzisha na Tizeba

Waziri wa Kilimo, Uvuvi na Mifugo, Dk Charles Tizeba

Muktasari:

Wakulima na mashirika yasiyo ya kiserikali wamekosoa uamuzi Dk Tizeba wa kupitisha kanuni mpya za uagizaji mbolea kwa mkupuo kupitia tangazo lake kwenye gazeti la Serikali Namba GN 49 ya mwaka 2017.

Dar es Salaam. Wakati vumbi kati ya wasafirishaji na Mamlaka ya Kusimamia Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra) likitulia kuhusu kanuni mpya, wadau wa kilimo wametifua jinsi dhidi ya Waziri wa Kilimo, Uvuvi na Mifugo, Dk Charles Tizeba kuhusu kanuni mpya za uingiza mbolea nchini.
Wakulima na mashirika yasiyo ya kiserikali wamekosoa uamuzi Dk Tizeba wa kupitisha kanuni mpya za uagizaji mbolea kwa mkupuo kupitia tangazo lake kwenye gazeti la Serikali Namba GN 49 ya mwaka 2017.
Kabla ya kusainiwa kwa kanuni hizo, kampuni za mbolea zimekuwa zikiagiza na kutengeneza kulingana na mahitaji ya wakulima.
Hata hivyo, alipoulizwa kwa njia ya simu kuhusu vifungu vya kanuni vinavyolalamikiwa, Waziri Tizeba alimtaka mwandishi kuzisoma upya kanuni hizo kabla ya kumuuliza maswali.
“Nimeyasikia (hayo malalamiko), naomba nijue wewe umeyasikia wapi,” aliandika Dk Tizeba kwa ujumbe mfupi wa simu.
 Akizungumzia kanuni hizo, Mkurugenzi wa Sera wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini, (TPSF), Gili Teri alisema Serikali imekuwa ikidai kuwa lengo la kanuni hizo ni kupunguza gharama za mbolea kwa wakulima bila kutaja kiwango.