Waliosaidia kuokoa manusura, waliofariki kulipwa Sh400,000

Muktasari:

  • Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasilino, Isaack Kamwelwe ametoa shukrani kwa waliojitolea katika ajali ya Kivuko cha Mv Nyerere kilichopinduka ziwa Victoria na kusema wote watalipwa kifuta jasho


Dar es Salaam. Serikali imesema kila aliyehusika katika shughuli ya kuokoa manusura na miili ya watu waliofariki katika ajali ya kupinduka kivuko cha MV Nyerere atapata kifuta jasho cha Sh400,000.

Mbali na kifuta jasho hicho, imeahidi kujenga wodi tatu za wanawake, wanaume na watoto katika Hospitali ya Bwisya wilaya Ukerewe jijini Mwanza pamoja na mnara wa kumbukumbu kwenye eneo la makaburi walipozikwa waliofariki katika ajali hiyo.

Fedha hizo zitakazotumika ni kati ya Sh946.6 milioni zilizokusanywa kama rambirambi kutokana na ajali ya kivuko cha Mv Nyerere kilichopinduka Septemba 20 na kupoteza maisha ya watu 228.

Akizungumza leo wakati wa kuhitimisha shughuli za uokoaji,  Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe alisema maamuzi hayo ni kutokana na maagizo ya Rais John Magufuli.

Alisema Rais aliagiza kuhakikisha kila aliyehusika wakiwamo wapishi, madereva wa gari ya wagonjwa na mitumbwi binafsi kulipwa kifuta jasho kwa kazi waliyoifanya.

Waziri huyo ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maafa hayo alisema mpaka sasa Sh689.9 milioni kati ya 946.6 zimebaki baada ya matumizi ya awali ikiwamo kulipa ndugu wa marehemu.

“Tunakisia matumizi ya kuwalipa Sh400,000 kila aliyehusika hayatavuka Sh240 milioni, hivyo fedha itakayobaki ndiyo itakayotumika kujenga wodi,” alisema.

Alisema Jumamosi ijayo saa 6:00 mchana itakuwa mwisho wa kutuma fedha za rambirambi kwa ajili ya maafa hayo ili kuepuka wizi unaoweza kufanywa na baadhi ya watu kuendelea kuchangisha.

Alisema tayari wamefikia hatua ya mwisho ya uokoaji japo kamati ya Ulinzi na usalama ya mkoa huo itaendelea kupiga kambi kuhakikisha eneo hilo linakuwa salama.

Kamwelwe aliwashukuru Watanzania, taasisi na wataalamu mbalimbali walioshiriki katika shughuli hiyo kwa namna moja au nyingine tangu siku ya kwanza ajali hiyo ilipotokea.