Waliotegemea foleni Tazara waendelea kukimbia flyover

Muktasari:

  • Kabla ya kujengwa kwa barabara hizo shughuli za biashara katika eneo hilo zilikuwa zimeshika kasi.

Dar es Salaam. Barabara za juu (flyover), zilizopo katika makutano ya barabara za Nyerere na Mandela eneo la Tazara, zimeendelea kuwafanya madereva wa bodaboda na wachuuzi wa bidhaa mbalimbali kukimbia sehemu hiyo.

Kabla ya kujengwa kwa barabara hizo shughuli za biashara katika eneo hilo zilikuwa zimeshika kasi.

Hivi karibuni madereva wa magari binafsi na daladala walisema walikuwa wakitumia hadi dakika 90 kuruhusiwa kupita eneo hilo kutoka upande mmoja hadi mwingine kabla ya barabara hizo za juu kuanza kutumika.

Kutokana na mazingira hayo ya foleni, wafanyabiashara walitumia fursa hiyo kufanya biashara kwa abiria wanaotumia daladala na magari binafsi yaliyokuwa yakikaa muda mrefu katika eneo hilo.

Madereva wa bodaboda nao walitumia fursa ya foleni kupakia abiria wenye haraka ya kuwahi katika shughuli zao waliokuwa wakishukia eneo hilo.

Jana, Mwananchi lilitembelea eneo la makutano ya barabara hizo na kukuta kituo mojawapo cha kusubiria abiria kikiwa na madereva wawili wa bodaboda.

“Wengi wamehama hapa kwa sababu hakuna biashara tena maana daladala hazikai sana kwenye foleni na nyingi zinapita huko juu kwenye flyover,” alisema dereva wa bodaboda Andrew Petro, aliyesema wengi wamehamia eneo la Buguruni.

“Hii barabara imetufukuzia wateja. Awali nilikuwa na uhakika wa kuingiza kati ya Sh30,000 hadi Sh40,000 kwa siku, lakini sasa hivi kuipata Sh20,000 ni mbinde (vigumu).”

Wachuuzi wa bidhaa

Wachuuzi wa bidhaa ndogondogo yakiwamo maji ya kunywa ya chupa walisema kumalizika kwa ujenzi wa barabara hiyo kumewafanya wengi wao kuondoka eneo hilo. “Ilikuwa ni kawaida kupata Sh70,000 au Sh80,000 kwa mauzo ya siku hasa kwenye foleni ya Tazara, lakini kwa sasa ni vigumu hata kupata Sh50,000,” alisema Frank James, mmoja wa wachuuzi wa bidhaa hizo.

Barabara hiyo iliyoanza kufanya kazi Septemba 15, inatarajia kuzinduliwa Oktoba na Rais John Magufuli ambaye pia ndiye aliweka jiwe la ujenzi wake Aprili 16, 2016.

Kwa mujibu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), kukamilika kwa mradi huo kutapunguza muda wa kukaa kwenye foleni kwa asilimia 80.