Naibu waziri aagiza waliovamia eneo la mnada kuondolewa

Muktasari:

Naibu waziri ameagiza kutengenezwa kisima kilichopo mnadani ili kupunguza gharama za maji.

Dodoma. Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega ameiagiza Manispaa ya Dodoma Mjini kuwaondoa watu waliovamia mnada wa upili wa Kizota ili kuwezesha utaratibu wa kisheria wa biashara ya mifugo na uchakataji kufanyika.

Akizungumza akiwa ziarani katika mnada huo unaomilikiwa na wizara hiyo, Ulega amesema wamelipa Sh20 milioni kwa ajili ya kuwaondoa waliovamia eneo hilo.

“Msimamo wa wizara ni lazima wakazi waliovamia mnada huu wa upili wa Kizota waondoke. Tumeshafanya hatua za kutoa Sh20 milioni kwa manispaa. Nyumba zilizopo hazizidi 200 labda zilizoko nje ya eneo letu,” amesema.

Amesema uwepo wa ardhi hiyo ni matakwa ya sheria inayotaka mifugo ipumzike na kula chakula kabla ya kukaguliwa, kwenda mnadani na baadaye kwenye viwanda vya uchakataji.

Ulega amesema manispaa wakutane na waliovamia eneo hilo na kuandaa utaratibu utakaowafanya waondoke.

“Watoe muda mfupi kwa watu kujipanga kwenda eneo jingine kabla halijaingia kwenye hatua iliyo ngumu,” amesema.

Ulega ametaka kutengenezwa kisima kilichopo eneo hilo ili kupunguza gharama za maji yanayotumiwa mnadani.

Amesema maji yanayozalishwa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (Duwasa) ni gharama kubwa ambayo ingeweza kuepukwa iwapo kisima hicho kitatengenezwa.

Hivi karibuni wafanyabiashara wanaopitishia mifugo katika mnada huo walimlalamikia Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge kuhusu fedha nyingi wanazotumia kuagiza maji kwa ajili ya mifugo yao.