Wanachuo Dodoma wadaiwa kujiuza kwa kutumia picha

Muktasari:

Kauli hiyo ilitolewa jana na Mkurugenzi wa Afnet, Sara Mwaga alipokuwa akizungumza kuhusu maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia kwa Kanda ya Kati ambayo kaulimbiu yake ni ‘Funguka, chukua hatua, mlinde mtoto apate elimu.’

Dodoma. Mtandao wa Wanawake Tanzania (Afnet), umetoa ripoti Polisi ukidai kuna udalali wa biashara ya ngono kwa wanafunzi wa vyuo kadhaa vya Dodoma unaofanywa na mameneja wa hoteli zilizopo katikati ya mji.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Mkurugenzi wa Afnet, Sara Mwaga alipokuwa akizungumza kuhusu maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia kwa Kanda ya Kati ambayo kaulimbiu yake ni ‘Funguka, chukua hatua, mlinde mtoto apate elimu.’

“Tumepata taarifa ziko baadhi ya hoteli hapa mjini ambazo watoto wetu wa vyuo wamepeleka picha zao kwa mameneja anapokuja mteja anahitaji huduma ya msichana anaonyeshwa zile picha”, alisema na kuongeza: “Akichagua anapigiwa simu kama yuko wapi anapanda bodaboda ndani ya dakika 10 au 20 anamhudumia mteja anarudi.”

Alisema hayo mbele ya Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, Ernest Kimola na maofisa wengine wa jeshi hilo na wawakilishi wa Mtandao wa Kupambana na Ukatili wa Kijinsia (Mkuki).

“Vijana wa chuoni wako katika mazingira hatarishi kwani wengi wao huenda shule wakiwa hawana fedha kutokana na umaskini wa familia zao. Sasa mikopo inapocheleweshwa au kutopatikana kabisa huwaweka katika mazingira hatarishi ya kushawishiwa kimapenzi,” alisema.

Alisema hali hiyo inawafanya wengine kufikia hatua ya kuuza miili yao ili wapate fedha na vitu vingine.

Alisema kupitia maadhimisho hayo, wanatoa wito kwa wadau wote wa elimu kuchukua hatua ili kuwalinda watoto na kuweka katika mazingira rafiki kwa utoaji wa elimu kuanzia msingi, sekondari hadi vyuoni.

“Tunaamini kupitia midahalo, majadiliano redioni, maonyesho ya video na shughuli nyingine, wadau watachambua kwa makini masuala haya na kuona au kupanga nini kifanyike ili kuleta mabadiliko chanya,” alisema.

Akizungumzia suala hilo Kamanda Kimola alisema: “Tuna njia nyingi za kupata taarifa. Tunawashukuru kwa kutupa taarifa.”

Alisema vitendo vya unyanyasaji na ukatili vinapokithiri huathiri ustawi wa jamii kuanzia ngazi ya familia.

“Kwa mfano mtoto ambaye anaishi na familia yenye ukatili hawezi kufanya vizuri katika masomo.

Mwenyekiti wa Chama cha Wenye Hoteli Mkoa wa Dodoma, Chavuma Haruna alisema hajawahi kupata taarifa za kuwapo kwa biashara hiyo. “Wewe ndiyo unaniambia sasa. Tutafuatilia na tunaomba ushirikiano kwa wakazi wa Mkoa wa Dodoma ili kwa pamoja tupeane mrejesho baada ya kfuatilia,” alisema.

Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Julian Bruno alisema hajawahi kusikia suala hilo chuoni hapo.

Alisema Udom kina wanafunzi wapatao 30,000 wanaojitambua, hivyo hawawezi kujihusisha na biashara hiyo.

Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo cha Mipango, Omary Mwanga naye alisema hajawahi kusikia jambo hilo.

Hata hivyo, alisema baada ya kuuliza kwa wenzake amepata taarifa kuwa kuna baadhi ya saluni mjini hapa ni mawakala (wanafunzi wa vyuo) ambao hufanya kazi ya kuwatafutia wanaume wanafunzi wenzao.