Wanafunzi 14 waliojeruhiwa na radi watoka hospitali

Muktasari:

  • Wanafunzi hao 14 kati ya 21 wa Shule ya Msingi Emaco Vision walilazwa hospitali ya Mkoa wa Geita baada ya kupigwa na radi

Geita. Wanafunzi 14 kati ya 21 wa Shule ya Msingi Emaco Vision waliokuwa wamelazwa katika hospitali ya Mkoa wa Geita baada ya kupigwa na radi wakiwa darasani wameruhusiwa kutoka hospitali

Tukio la wanafunzi kupigwa radi mjini Geita lililotokea jana Jumatano Oktoba 17, 2018 wakati wanafunzi hao wakiwa darasani, lilisababisha wanafunzi sita kufariki dunia na kujeruhi 21 na walimu wawili.

Akizungumza na MCL Digital leo Oktoba 18, 2018 kaimu mganga mfawidhi wa hospitali hiyo, Moses Simon amesema wanafunzi wengi wamepata majeraha ya miguuni na shingoni.

Dk Simon amesema mwalimu mmoja amejeruhiwa zaidi baada ya kuungua sehemu kubwa ya mwili wake na bado wanaendelea kumpatia matibabu.

Mwalimu wa shule hiyo, Edward Bartholomeo amesema wamesitisha kufundisha kwa muda na wataendelea na masomo Jumatatu Oktoba 22.

Amesema baadhi ya wanafunzi waliofariki dunia walizikwa jana wengine watazikwa kesho Jumamosi.