Wanafunzi 26 wasimamishwa masomo kwa kupata mimba

Muktasari:

Mradi wa Tuwalinde unatekelezwa katika wilaya ya Hai, lengo ni kuhamasisha jamii kuwalinda watoto wa kike dhidi ya mimba na ndoa za utotoni.

Katika kipindi cha Januari hadi Septemba, 2018, wanafunzi 26 wamepata ujauzito

Hai. Wanafunzi 26 katika halmashauri ya wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, wamesitisha masomo yao katika kipindi cha Januari hadi Septemba, 2018 baada ya kupata ujauzito huku 11 kati yao wakiwa ni wanafunzi wa kidato cha nne.

Kufuatia hali hiyo, halmashauri hiyo imepiga marufuku wanafunzi kuhudhuria sherehe za usiku kuanzia saa 12 jioni, kwa madai zimekuwa chanzo kikubwa cha watoto wa kike kurubuniwa na kupata ujauzito.

Hayo yalibainishwa jana Septemba 25, 2018 na ofisa takwimu idara ya elimu sekondari, Salome Msegeya wakati akitoa taarifa kwenye mkutano wa wadau mbalimbali uliokuwa ukijadili masuala ya kumlinda mtoto wa kike na kutokomeza mimba za utotoni, ikiwa ni utekelezaji wa mradi wa Tuwalinde, unaotekelezwa wilayani Hai, kata ya Kia na Masama Rundugai na Shirika la Ajiso.

Msegeya alisema pamoja na jitihada mbalimbali ambazo wamekuwa wakizichukua katika kuhakikisha wanamlinda mtoto wa kike, bado kumekuwepo na wasichana wanaokatisha masomo yao kutokana na kupata ujauzito, jambo ambalo limekuwa likizima ndoto zao.

“Wanafunzi 26 wamepata ujauzito na kati yao 11 ni wa kidato cha nne, hili linasikitisha sana, maana tulitegemea wanafunzi wa kidato cha nne tayari wamejitambua na wameruka vikwazo vingi, lakini wamekuja kukatisha masomo wakiwa kwenye hatua za mwisho” alisema.

kuhusu marufuku ya wanafunzi kushiriki sherehe, Msegeya alisema, wanafunzi hawataruhusiwa kushiriki sherehe yoyote kuanzia saa 12 jioni na kwamba tayari wametoa taarifa kwa viongozi mbalimbali wa Serikali, kuwakamata wanafunzi watakaoonekana kwenye sherehe usiku.

Mwalimu wa Shule ya Msingi Chemka, John Mbwambo alisema wazazi wamekuwa chanzo cha watoto wa kike kujiingiza kwenye mahusiano ya kimapenzi katika umri mdogo na kupata ujauzito. 

“Kuna wazazi mtoto wao anapata ujauzito au anaonekana kubadilika kitabia, wao wanasimama kuwatetea na kulalamikia walimu kufuatilia watoto wao, hili ni tatizo linalochangia mimba za utotoni, wazazi na walezi lazima tuwe makini,” alisema Mbwambo. 

Mkurugenzi Mtendaji wa shirika lisilokuwa la kiserikali linalojihusisha na utetezi wa haki za binadamu na utoaji ushauri wa kisheria kwa makundi mbalimbali katika jamii (Ajiso), Virginia Silayo, alisema ni jukumu la kila mwanajamii kumlinda mtoto wa kike na kuhakikisha tatizo la mimba za utotoni linakwisha.