Wapigania uhuru Catalonia wakamatwa

Muktasari:

Wanaharakati hao wanafanyiwa uchunguzi kuhusu maandamano ya Septemba 20, ambayo kutokana na umati mkubwa walizuia maofisa wa Ulinzi wa Raia ndani ya jengo huko Barcelona mji wa mkuu wa Catalonia.

Barcelona, Hispania. Viongozi wawili mashuhuri wa makundi yanayoendesha harakati za eneo la Catalonia kujitenga, Jordi Sanchez na Jord Cuixart viongozi wametiwa ndani na wanashikiliwa bila ya dhamana wakati wakifanyiwa uchunguzi wa madai ya uchochezi.

Watu hawa walikuwa vinara katika upigaji wa kura ya kudai uhuru Oktoba Mosi, mchakato ambao Serikali ya Hispania inachukulia kuwa ni haramu. 

Kizuiwa kwa vinara hao kulisababisha maandamano usiku kucha, na mengine yanatarajiwa kufanyika maeneo yote ya Catalonia leo Jumanne.

Sánchez, ambaye ni Rais wa Baraza la Catalonia (ANC), taasisi inayounga mkono uhuru wa eneo hilo na Cuixart, na kiongozi wa taasisi ya kitamaduni ya Omnium, walifikishwa Mahakama Kuu jijini Madrid Jumatatu.

Wanaharakati hao wanafanyiwa uchunguzi kuhusu maandamano ya Septemba 20, ambayo kutokana na umati mkubwa walizuia maofisa wa Ulinzi wa Raia ndani ya jengo huko Barcelona mji wa mkuu wa Catalonia.

Kutokana na kura ya maoni, kiongozi wa Catalan Carles Puigdemont alitia saini tamko la uhuru, lakini alisitisha utekelezaji wake ili kuruhusu mazungumzo na Serikali ya Hispania. Puigdemont ametoa wito mazungumzo yafanyike ndani ya miezi miwili ijayo.

Hata hivyo, Serikali ya Hispani imewataka viongozi wa Catalonia kubatilisha tamko lao vinginevyo watatawaliwa moja kwa moja kutoka Madrid. Jumatatu Puigdemont aliwakasirisha Madrid kwa kukataa kufafanua kama alitangaza uhuru wiki iliyopita au la.

Puigdemont, akiyepewa muda kufafanua nafasi yake ifikapo Alhamisi amelaani kushikiliwa na viongozi hao. "Serikali ya Hispania imewafunga wanaharakati wa asasi za kijamii wa Catalonia kwa kusimamia maandamano ya amani. Inasikitisha kwamba sasa tunawafungwa wa kisiasa," amesema.