Thursday, July 13, 2017

Wananchi 300 wajiunga na mpango wa hiari

“Kuwa na bima ya afya ni muhimu lakini kuchagua

“Kuwa na bima ya afya ni muhimu lakini kuchagua mfuko wa bima hiyo ni muhimu zaidi.” Risasi 

By Kalunde Jamal, Mwananchi kjamal@mwananchi.co.tz

 Dar es Salaam. Mfuko wa Pensheni wa PSPF umesajili wananchi 301 katika mpango wa uchangiaji wa hiari utakaowezesha wanachama kupata huduma za hifadhi ya jamii.

Akizungumza jana katika Maonyesho ya 41 ya kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (DITF), Ofisa Uhusiano Mwandamizi wa PSPF, Abdul Njaidi alisema wengi waliosajiliwa wanataka kupata huduma ya matibabu.

Alisema kwa kutumia maonyesho hayo, PSPF imetoa huduma kwa wananchi wapatao 500, waliofika katika banda hilo wakiwa na mambo mbalimbali yanayohitaji huduma.

“Wananchi wengi waliofika katika banda hili wanaonyesha ni kwa namna gani wanapenda huduma za afya,” alisema Njaidi.

Alifafanua kuwa waliohitaji walisajiliwa ili kuendelea kuchangia kwa hiari.

Njaidi alisema PSPF inampongeza, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango kwa jitihada alizozionesha za kujiunga na mpango huo wa hiari, jambo litakaloongeza elimu kwa wananchi kuhusu mpango huo na manufaa yake.

Njaidi aliwasihi wananchi wasiokuwa katika sekta rasmi kuingia katika mpango huo, wakitambua kuwa fedha wanazochangia ni za kwao.

Alisema wakijiunga watakuwa huru kuchagua jinsi ya kuwasilisha michango yao ikiwa ni pamoja na kwa mwezi, wiki au msimu.

Njaidi alisema mafao ya mpango huo, mwanachama atalipwa michango na faida itakayopatika kutokana na uwekezaji.

Mmoja wa waliojiunga na mpango huo, Jovin Risasi alisema amevutiwa baada ya kuona picha ikimuonyesha Dk Mpango akiwa anajiunga.

Alidai kuwa mpango huo unaowalenga wananchi walioajiriwa na waliojiajiri katika sekta isiyo rasmi na sekta rasmi, umewagusa watu wengi.

-->