Wananchi wachukua maiti na kuibwaga kituo cha polisi

Wananchi wa Kijiji cha Puma wilayani Ikungi wakiwa wamekusanyika katika Kituo cha Polisi kijijini hapo  baada ya kupeleka mwili wa Easter Ndahani anayedaiwa kuuawa kwa kuchomwa na kitu chenye ncha kali kifuani, mkoani Singida juzi. Na Mpigapicha Maalum

Muktasari:

Wananchi hao waliandamana baada ya askari wa kituo hicho, PC Lucas kudaiwa kugoma kumkamata mtuhumiwa anayedaiwa kusababisha mauaji hayo, bila kupewa Sh10,000 ya usafiri.

Wananchi wa Kijiji cha Puma wilayani Ikungi katika Mkoa wa Singida wameandamana hadi kituo cha Polisi cha Puma wakiwa wamebeba maiti ya mwanamke aliyekuwa mkazi wa kijiji hicho, Ester Ndahani aliyeuawa kwa kuchomwa na ‘bisibisi kifuani karibu na kwenye ziwa na kuibwaga.

Wananchi hao waliandamana baada ya askari wa kituo hicho, PC Lucas kudaiwa kugoma kumkamata mtuhumiwa anayedaiwa kusababisha mauaji hayo, bila kupewa Sh10,000 ya usafiri.

Huo ni mwendeleo wa wananchi kuchukua hatua dhidi ya matukio ya mauaji kwani hivi karibuni wananchi wa Mtaa wa Nyakabale, Geita, waliuchukua mwili wa marehemu Zakaria Shabani na kwenda kuutelekeza nyumbani kwa mwenyekiti wa mtaa, Elias Ndalawa wakimtuhumu kutoshughulikia tukio la marehemu kupigwa na polisi jamii hadi kufa.

Katika tukio hilo, wananchi hao waliuweka mwili huo kitandani kwa mwenyekiti huyo na kisha kushusha chandarua.

Katika tukio la Ndahani, Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Miraji Mtaturu alisema kibaya zaidi, wanakijiji hao walitumia mgambo kumkamata mtuhumiwa huyo na baada ya kumfikisha polisi aliachiwa baadaye kinyume cha sheria.

Alisema baada ya mwanamke huyo kuchomwa alikwenda polisi na kupewa hati ya matibabu ‘PF3’, lakini hakuweza kutibiwa baada ya kufikishwa zahanati kwa kukosa fedha na bima ya afya.

Mtaturu alisema mgonjwa huyo aliamua kurejea nyumbani na majeraha yake hadi alipofariki dunia kwa sababu ya uzembe wa polisi na zahanati ya kijiji.

Alisema baada ya mwanamke huyo kufariki, wananchi waliamua kubeba maiti na kwenda kuitelekeza kwenye kituo cha polisi wakitaka viongozi wa juu kufika kutoa majibu ya kilichotokea kabla kuzika.

“Haiwezekani mtumishi wa umma ushindwe kutimiza wajibu wako ipasavyo na kusababisha uhai wa mtu upotee kwa sababu hakuna pesa, kilichotokea kwa hawa watumishi wa umma hakikubaliki hata kidogo,” alisema.

Alimuagiza mkuu wa polisi wa wilaya hiyo kumkamata, kuweka chini ya ulinzi na kumfanyia mahojiano mganga mkuu wa zahanati hiyo kwa kosa la kutomtaja aliyekuwa zamu wakati mgonjwa alipofikishwa.

Pia aliagiza askari aliyeshindwa kutimiza wajibu wake akamatwe, kuhojiwa na kusimishwa kazi wakati uchunguzi juu ya tuhuma zake ukiendelea.

“Kwa sababu huyu mganga wa zahanati hajaleta jina la nani alikuwa zamu siku hiyo, OCD mkamate na muweke ndani ili ataje ni nani alikuwepo siku ile akashindwa kumhudumia mgonjwa aliyefikishwa huku akivuja damu,” alisema na kuongeza;

“Hata kama mtu huyu hana pesa wala bima ya afya kipo kifungu cha sheria kinachotoa msamaha wa matibabu kwa wasio na uwezo. Hivi mgonjwa akiletwa hoi tena anavuja damu utamuacha kwa sababu hana pesa! Haya ni maadili ya wapi? Watumishi wa aina hii ndio ambao wanachafua taswira ya Serikali, hatutakubali hata kidogo.”

Mtaturu alisema ni wajibu wa Serikali kuhakikisha wananchi wake wanakuwa na afya hivyo kitendo cha mgonjwa huyo kutotibiwa wakati alifika akiwa na hali mbaya ni kosa.

“Ninachotaka ni kupata ukweli wa kila kitu, nijue kwa nini huyu askari alishaletewa hadi mtuhumiwa lakini hakutaka kushughulikia jambo hili kwa wakati. Poleni sana wananchi kwa msiba na sisi Serikali hili suala tunaendelea kulifanyia kazi. Ni haki yenu kuwa salama na kuhudumiwa kwa mujibu wa sheria,” alisema.

Pia Mtaturu aliagiza utaratibu ufanyike ili kituo hicho cha polisi kianze kutoa huduma kwa wakati wote huku akiwasisitiza askari kuwa waaminifu.

Baada ya mkuu huyo wa wilaya kuzungumza na wananchi hao, walioundoa mwili huo.

Baadhi ya wananchi waliozungumzia suala hilo walisema kilichotokea ni uzembe na kwamba, hiyo ndiyo sababu iliyowafanya waandamane kuipeleka maiti kwenye kituo cha polisi.

Mmoja wa wananchi hao, Juma Wilimba alisema, “Tuliamua kuipeleka maiti hapo ili kuonyesha masikitiko na hasira zetu kwa watendaji hao wa Serikali. Tulitaka iwe mfano.”

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Deborah Magiligimba alisema mwanamke huyo alifika Kituo cha Polisi cha Puma Machi 9 na kupewa huduma za awali ikiwamo hati ya matibabu.

“Jana tumepata taarifa kwamba amefariki, kwa hiyo tunaendelea kufanya uchunguzi wa kina kuhusu malalamiko yote ya wananchi juu ya tukio hili,” alisema.

Hata hivyo, taarifa za lini atazikwa hazikuweza kupatikana.

Alipotakiwa kutoa maoni yake kuhusu tukio hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Dk Hellen Kijo-Bisimba alisema ni kosa kisheria kutompa matibabu mgonjwa aliyepata dharura ikiwamamo kupigwa na kuvuja damu, kwa sababu ya kukosa fedha.

“Ina maana huyu mama hakutibiwa kwa sababu hana pesa? Hii siyo sawa, kwa hiyo kama wananchi waliamua kuchukua hatua hiyo ya kuandamana ilikuwa haki yao kwa sababu wasingepata sehemu ya kupaza sauti zao kwa jambo lililotokea ambalo linavunja haki za binadamu,” alisema.