Wanasiasa Dodoma wawataka vijana kujipanga kifursa

Mbunge wa Dodoma Antony Mavunde

Muktasari:

Rai hiyo ilitolewa jana na madiwani na mbunge wa jimbo la Dodoma walipokuwa wakizungumza na vijana na wafanyabiashara wa Soko la Majengo mjini hapa.

Dodoma. Wanasiasa wa Dodoma wamezungumzia ujio wa makao makuu katika mkoa huo kama ni lulu kwao na wapiga kura wao, lakini wakataka vijana kujipanga zaidi.

Rai hiyo ilitolewa jana na madiwani na mbunge wa jimbo la Dodoma walipokuwa wakizungumza na vijana na wafanyabiashara wa Soko la Majengo mjini hapa.

Mbunge wa Dodoma Antony Mavunde aliwataka vijana kuwa makini na kujiandaa kikamilifu vinginevyo wataishia kuwa vibarua kwa wenzao watakaoziona fursa na kuzifuata Dodoma.

Mavunde ambaye pia ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu alisema katika mpango mkubwa wa Serikali wa kuwatengenezea fursa vijana zaidi ya milioni 4 na wale wa Dodoma watakuwamo.

Aliwataka vijana kuchangamka na kuanzisha vikundi vya ujasiriamali ili waweze kukopesheka na kwamba wasipofanya hivyo itakuwa ni vigumu kwa Serikali kuwafikia.

Diwani wa Kata ya Majengo Msinta Mayaoyao alisema kwa ujio wa makao makuu, mji wa Dodoma utapaa kiuchumi na vijana wengi watatengeneza ajira.

Mayaoyao alisema hivi sasa tayari biashara zimeanza kuchangamka kwa kiasi kikubwa na vijana wengi wamejipanga kutulia katika masoko na kutafuta bidhaa ambazo zinaendana na soko la wakati huu. “Hata hao wanaokuja waje tu, vijana hawana shaka na hilo na ndiyo maana unaona hata miundombinu inabadilishwa ili kuweka kila kitu vizuri, tumefurahi sana,” alisema Mayaoyao.

Diwani wa Kata ya Uhuru Ali Heri alisema mambo yote kwa sasa yako vizuri na kinachosubiriwa ni ugeni kuanza kuongezeka na watu wapate fursa ya kufanya kile wanachoona kinafaa.