Wanawake wauawa, wanyofolewa viungo

Muktasari:

  • Wakazi wawili wa Kijiji cha Lubanga mkoani Geita ambao ni mtu na shangazi yake, Kija Lushanga (70) na Pendo Bukelebe (48) wameuawa kwa kukatwa mapanga  mwishoni mwa wiki na watu wasiojulikana walioondoka na viungo vyao

Geita. Wakazi wawili wa Kijiji cha Lubanga mkoani Geita wameuawa kwa kukatwa mapanga na kunyofolewa viungo mbalimbali vya mwili, tukio linalodaiwa kufanywa na watu wasiojulikana walioondoka na viungo hivyo.

Kamanda wa polisi mkoani humo, Mponjoli Mwabulambo amesema tukio hilo limetokea mwishoni mwa wiki na waliouawa ni mtu na shangazi yake.

Amewataja waliouawa kuwa ni Kija Lushanga (70) na Pendo Bukelebe (48) ambapo alisema wauaji hao waliondoka na viungo hivyo.

Kufuatia mauaji hayo jeshi la polisi limewakamata watu wanne kwa mahojiano na kwamba uchunguzi bado unaendelea. 

Kamanda huyo hakuwa tayari kuwataja wanaoshikiliwa kwa uchunguzi kwa kile alichodai kitaharibu uchunguzi.

Alisema jamii inayozunguka eneo hilo inahusisha mauaji hayo na imani za kishirikina lakini wao kama jeshi la polisi kwa sasa wanachukulia kuwa ni mauaji isipokuwa watakapokamilisha uchunguzi ndio wataweza kujua nini kiini cha mauaji na watu kuondoka na viungo hivyo.

“Ni mapema kujua chanzo cha mauaji haya watu wamezoea kufananisha mauaji ya aina hii na ushirikina, lakini sisi tunachunguza na hata sasa licha ya hawa tuliowakamata bado wapo wengine tunawasaka na tukishawakamata tutabaini nini kipo nyuma ya mauaji haya,” alisema Mponjoli.

Mkoa wa Geita ni miongoni mwa mikoa yenye matukio ya mauaji ya wanawake kukatwa mapanga. Mei 17, 2018 Sophia Sitta mkazi wa kijiji cha Mwabasabhi wilayani Chato aliuawa na mwili wake kutenganishwa kichwa na kiwiliwili.

April 05, 2018 wanawake wanne wilayani Nyang’hwale waliuawa kwa kunyongwa kisha miili yao kutupwa porini.

Juni 06 ,2018 polisi walimuua kwa kumpiga risasi Panda Kinasa (36) ambaye alikua akiteka watu kudai fedha kisha kuwaua.

Takwimu za polisi za mwaka 2015 zinaonyesha kuwa watu 32 walipoteza maisha mkoani Geita kwa kipindi cha miezi mitatu Oktoba-Disemba 2015 kutokana na mauji ya kutumia mapanga yanayodaiwa kusababishwa na imani za kishirikina.