Waratibu wa elimu Dar wamwagiwa neema ya pikipiki

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Selemani Jafo akiwa amembeba Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani (Necta), Dk Charles Msonde wakati wa hafla ya makabidhiano ya pikipiki 2894 zenye thamani ya shilingi bilioni 8.5 kwa waratibu wa elimu ngazi ya kata nchini iliyofanyika jijini Dar es Salaam leo. Picha na Ericky Boniphace

Muktasari:

  • Waaswa wasizifanye bodaboda

Dar es Salaam.Serikali imewakabidhi pikipiki 2894 waratibu wa elimu katika kata za nchi nzima kwa ajili ya kuboresha sekta hiyo na wamewataka kutozifanyia biashara ya bodaboda.

Pikipiki hizo zimekabidhiwa leo , Jumanne Julai 3 viwanja vya Mnazi Mmoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Seleman Jafo na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako.

Akizungumza kabla ya kukabidhi pikipiki hizo, Jafo aliwataka waratibu hao kuutumia usafiri huo kwa malengo yaliyokusudiwa ikiwamo kutembelea na kukagua shule zilizopo mbali.

"Pikipiki zina thamani ya zaidi ya Sh 8bilioni, naomba zitumike ipasavyo .Isitokee mkawakabidhi vijana ili jioni walete hesabu, tunataka mkasimamie taaluma hii,"amesema Jafo.

Kwa upande wake, Profesa Ndalichako amesema haijawahi kutokea kwa waratibu kukabidhiwa pikipiki na aliishukuru Serikali kwa namna itavyotekeleza ahadi zake kwa vitendo.

“Waratibu wa elimu msituangushe vitendea kazi ndiyo hivi.Sijui mtakuja na hadithi gani, naomba mkajitume," amesema Profesa Ndalichako.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema mkoa huo bado unaendelea na jitihada mbalimbali za kuwasaidia walimu ili watekeleze majukumu yao kwa ufanisi.

"Mawaziri wangu bado tunapambana kuboresha maslahi ya walimu, ikiwamo kusafiri bure.Walimu wa mkoa huo msiwe na wasiwasi fenicha zenu zipo,"amesema Makonda