Warithi wa Lissu wajipanga kuipangua TLS

Muktasari:

  • Lissu, ambaye anaendelea na matibabu nchini Ubelgiji alichaguliwa kuwa Rais wa TLS Machi 18 mwaka jana lakini alitumikia nafasi hiyo kwa takriban miezi sita baada ya Septemba 7 kushambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 na watu wasiojulikana akiwa nje ya makazi yake mjini Dodoma baada ya kutoka bungeni.

Dar es Salaam. Wakati Tundu Lissu akimaliza muda wake wa uongozi ndani ya Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) na kusema hakufanikiwa kukamilisha matarajio yake, wagombea wanaowania kumrithi wameahidi kufanya mabadiliko makubwa ikiwamo kuhamishia ofisi za chama hicho makao makuu ya nchi, Dodoma.

Lissu, ambaye anaendelea na matibabu nchini Ubelgiji alichaguliwa kuwa Rais wa TLS Machi 18 mwaka jana lakini alitumikia nafasi hiyo kwa takriban miezi sita baada ya Septemba 7 kushambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 na watu wasiojulikana akiwa nje ya makazi yake mjini Dodoma baada ya kutoka bungeni.

Baada ya shambulio hilo, alipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Dodoma na usiku wa siku hiyohiyo alihamishiwa Hospitali ya Nairobi ambako alilazwa hadi Januari 6 alipohamishiwa Ubelgiji kwa matibabu zaidi.

Tayari wanasheria wanne wamejitokeza kawania nafasi hiyo katika uchaguzi utakaofanyika Aprili 14 jijini Arusha, safari hii ukifanyika chini ya masharti mapya kwa wagombea tofauti na ilivyokuwa huko nyuma.

Masharti hayo ambayo yapo katika kanuni za uchaguzi huo kwenye Gazeti la Serikali (GN) namba 116 ya mwaka 2018, kipengele cha (8) (e) kinaeleza kuwa mwanachama anayetaka kugombea asiwe mtumishi wa umma, mbunge, diwani au hatakuwa kiongozi wa chama cha siasa kilichosajiliwa.

Wanasheria waliojitokeza kuwania urais ni Fatma Karume, Godwin Ngwilimi, Godwin Mussa na Godfrey Wasonga. Aliyepitishwa na kamati ya uchaguzi ya TLS chini ya mwenyekiti wake, Dk Kibuta Ongwamuhana kuwania umakamu wa rais ni Rugemeleza Nshalla.

Ahadi za wagombea

Akizungumzia sababu za kuwania nafasi hiyo, Mussa alisema: “TLS kwa sasa inahitaji kiongozi atayeweka wanachama pamoja kwa kuwaunganisha na kupunguza tofauti ili inapofanya jambo, linakuwa la pamoja na wanachama wanaishi kuendana na taaluma yao ya sheria na si vinginevyo.

“TLS ilipoanzishwa mwaka 1954, ilikuwa na malengo yake na moja ni kuishauri Serikali katika masuala ya sheria, lakini hili limepotea kabisa na linahitaji kufanyiwa kazi. Lakini lengo jingine lilikuwa ni kutoa msaada kwa wanyonge wanaohitaji haki ila kutokana na unyonge wao hawakuweza, sasa nitahakikisha hili linafanyika.”

Mussa alisema atahakikisha anarejesha uhusiano kati ya taasisi hiyo na Serikali; “Na Serikali ione TLS ni mdau muhimu na TLS ione Serikali nayo ni mdau muhimu pia kwani hakuna Serikali yoyote duniani inayokubali kuona chombo chake kikienda visivyo ikakubali.”

Alisema kukiwa na mazingira mazuri kati ya TLS na wadau wengine, hata misuguano ya hapa na pale haitakuwapo na Serikali itapokea ushauri kutoka kwa wanasheria kama lengo lake tofauti na ilivyo sasa akisema inaweza isiuchukue hata kama ni mzuri.

Kuhusu masharti ya mwaka huu ya kuwaengua wanasiasa na watumishi wa umma, Mussa alisema, “Hili linazungumzika, TLS inaendeshwa kwa misingi yake, hata kama mtu ana cheo huko hakiwezi kuathiri na kwa kuwa Baraza la Uongozi lipo, nafikiri hawezi kuathiri kwa hiyo hili nikifanikiwa kushinda nitalifanyia kazi tusiwanyime fursa watu.”

Mgombea mwingine, Fatma Karume alisema, “Uongozi wa Tundu umekatizwa kwa kitendo cha uhalifu. Ukitazama uongozi wa Tundu umekuwa mfupi sana, hajaweza kutimiza yale aliyotaka kutimiza si kwa matakwa yake ila waliotaka kumuua.”

Fatma ambaye ni mtoto wa Rais mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume alisema kuna watu wengi hawajui haki zao na sheria hivyo ni wajibu wa TLS kuwasaidia na kuhakikisha sheria za nchi zinaheshimiwa na kila mmoja.

“Nitahakikisha TLS tunajali wanachama wetu, tunawajali wanasheria wetu kwa sababu hiyo ni muhimu sana. Huwezi kumpenda mtu wa nje kama wewe hujipendi ni muhimu kukaa pamoja, tupendane halafu tuhakikishe tunawasaidia wananchi,” alisema.

Alisema hategemei ndani ya mwaka mmoja akamaliza kila kitu lakini, “Nitahakikisha nawasha taa kidogo watu waone na mtu mwingine atakuja na kuendelea kwani mtu mmoja huwezi kumaliza kila kitu kwa mwaka mmoja.”

Wakati Fatma akisema hayo, Wasonga alisema: “Nimejipanga vizuri tu na endapo nikipewa nafasi ya kuwa kiongozi, kuna vitu naviona haviko sawa hasa huu uchaguzi. Kila mwaka unaendeshwa, ili kupunguza gharama, kuna haja ya kuishawishi Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali tuibadili Sheria ya TLS ili kiongozi akae miaka miwili au mitatu.”

Alisema kutokana na ongezeko la mawakili ambao sasa wako takriban 6,000 anaona hakuna haja kila mwaka kukutana wote katika mkutano mkuu hivyo atapendekeza kuwapo kwa wawakilishi ili kupunguza gharama.

Wasonga alisema anachokiona sasa, TLS inahitaji maboresho ya sheria ili kwenda na kasi ya teknolojia akisema, “Tunakwenda mbali, tumekuwa kama chama cha siasa, sasa turudi katika malengo ya kuanzishwa kwa TLS na mimi nataka kulifanya hilo. Sisi kazi yetu ni kuisaidia jamii ya Watanzania katika masuala ya sheria, tuwasemee wananchi katika mambo ya shida, tuikosoe Serikali pale taratibu zinapovunjwa bila kukiuka maadili ya taaluma yetu.

“Mimi nataka kuondoa ‘tension’ iliyopo kati ya TLS na Serikali kwa sababu TLS imeanzishwa na sheria kwa hiyo ni mali ya Serikali. Kwa hiyo nataka kuondoa uadui uliopo ili Serikali iweze kuwa karibu nasi bila kuathiri nafasi ya mtu yoyote.”

Wasonga alisema wadau wakuu wa TLS ni Serikali na Mahakama ambazo zote zinahamia Dodoma; “Na mimi kwa kuwa ni mwenyeji wa Dodoma, kwa hiyo hatuwezi kujitenga na wadau wetu, hivyo wakinipa nafasi nitaanza utaratibu wa kuihamishia TLS mkoani Dodoma.”

Wakati wagombea wenzake wakijinadi Ngwilimi ambaye sasa ni makamu wa rais, alisema hawezi kuzungumza lolote kwa sasa kwani kampeni hazijaanza na kwamba zikianza atafanya hivyo.

Hata hivyo, baadhi ya wagombea wenzake walipinga kauli hiyo wakisema kampeni hizo zimeshaanza huku Wasonga akithibitisha kwa kusema; “kampeni zimeshaanza na mimi Jumatatu nitafanya mkutano mkubwa sana na waandishi hapa Dodoma.”

Mgombea mwingine aliyezungumzia suala la kuanza kwa kampeni ni Mussa ambaye alisema, “Kwa kawaida kampeni rasmi huanza siku moja kabla ya uchaguzi lakini kwa sasa ni zile za kawaida tu kama hizi ambazo tumeongea.”

Kauli ya Lissu

Jana, Lissu akizungumza na mwandishi wetu alisema: “Nilipoomba kuchaguliwa na baada ya kuchaguliwa, ile siku niliyochaguliwa (Machi 18, 2017), katika hotuba yangu baada ya kuchukua mikoba rasmi, nilielezea changamoto kubwa zinazokaibili nchi na TLS kwa sababu mawakili ni sehemu ya jamii.

“Matatizo ya jamii ni matatizo ya TLS na nilisema hizo changamoto hazitanyamaziwa katika mwaka wangu mmoja wa kuwa rais, lakini nimekuwa rais kwa miezi mitano. Katika hiyo miezi mitano nilijaribu kwa kiasi kikubwa kutimiza kile nilichoahidi.”

Lissu ambaye pia ni mbunge wa Singida Mashariki alisema: “Hatukunyamaza, TLS yangu haikunyamaza, tulizungumza palipohitaji kuzungumza, tulipiga kelele tulipohitaji kupiga kelele, kilikuwa ni kipindi chenye changamoto kubwa sana.”

“Tuliitisha mkutano wa dharura na kuja wazi kabisa kuwa hatutakubali TLS kuwa chini ya mamlaka ya Serikali.”

Lissu alisema tofauti na miaka ya nyuma ambayo mambo yalikuwa yanafanyika na TLS imejificha, “TLS ya miezi mitano hatukujificha uvunguni.”

Alisema hayo ni miongoni mwa yale anayojivunia.