Watanzania, wageni wadaiwa kushirikiana matukio ya ugaidi
Muktasari:
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni ameyasema hayo wakati akifungua kikao cha saba cha Baraza la Utekelezaji la Wafanyakazi wa Idara ya Polisi.
Dar es Salaam. Ushirikiano mbaya kati ya baadhi ya Watanzania na wageni wenye nia mbaya umeibua sintofahamu inayosababisha viwapo viashiria vya ugaidi hapa nchini.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni ameyasema hayo wakati akifungua kikao cha saba cha Baraza la Utekelezaji la Wafanyakazi wa Idara ya Polisi.
“Upo uwezekano mkubwa wanaotekeleza uhalifu huo wanapitia katika mafunzo yasiyo rasmi ndani na nje ya nchi na yanahusisha matumizi ya silaha na mbinu mbalimbali za kisayansi zinazowasaidia kutekeleza uhalifu huo,” amesema
Masauni amesema zipo kambi zinazotumika kama maficho ya siri yanayowawezesha watu hao kutekeleza uovu na imeshuhudiwa kuibuka kwa matukio mbalimbali yenye viashiria hivyo ikiwamo kuvamiwa kwa vituo vya polisi.
“Lazima tuimarishe mikakati yetu ya kukabiliana na matukio haya ya kidhalimu kwa maslahi na ustawi wa watu wetu na Taifa na tunataka muafaka wa kubaini kusambaratisha na kuondoa mitandao inayojihusisha na matukio ya aina hii bila ya kuionea haya wala huruma,”amesema.
Mwenyekiti wa wa baraza hilo, Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi, Abdulrahman Kaniki amesema wanakabiliwa na changamoto ya ufinyu wa bajeti ambao unasababisha utekelezaji wa majukumu yao kuwa mgumu .
“Hizi changamoto tunazileta rasmi baada ya maazimio ya Baraza la Utekelezaji la Wafanyakazi wa Idara ya Polisi tutakapofikiana,”amesema Kaniki.