Wednesday, January 11, 2017

Watoto 10,000 huzaliwa na selimundu nchiniNaibu Waziri wa Afya, Dk Hamis Kigwangalla

Naibu Waziri wa Afya, Dk Hamis Kigwangalla 

By Herieth Makwetta, Mwananchi hmakweta@mwananchi.co.tz

 Dar es Salaam.. Watoto kati ya 8,000 hadi 11,000 huzaliwa nchini kila mwaka kutokana na tatizo la selimundu

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kifaa kipya cha kupima ugonjwa huo cha Sickle Scan, Naibu Waziri wa Afya, Dk Hamis Kigwangalla amesema kitatumiwa na kutoa majibu yenye ubora.

 Amesema takwimu za kidunia zinaonyesha watoto 312,307 wanazaliwa na tatizo la selimundu kila mwaka na asilimia 76 kati yao huzaliwa Afrika.

 Dk Kigwangallah amesema kwa kutambua tatizo hilo wizara imekuwa ikiweka  mikakati kuhakikisha linapatiwa ufumbuzi katika upimaji hadi kwa watoto wachanga wanaozaliwa nao.

 “Lengo la Serikali ni kuongeza nafasi za kuishi kwa wagonjwa kwa zaidi ya asilimia 20, tofauti na tulipo sasa, kuboresha huduma za uchunguzi na matibabu na kuongeza uelewa kwa jamii juu ya tatizo hili,” ameema Kigwangalla.

 Kifaa hicho kina uwezo wa kugundua aina mbalimbali za selimundu kwa teknolojia rahisi isiyohitaji matumizi ya umeme, ikilinganishwa na vifaa ambavyo vimekuwa vikitumika nchini.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Medomix Concept inayosambaza kifaa hicho, Pristilla Karobia amesema wameamua kuleta vifaa hivyo kwa ajili ya kukabiliana na tatizo la Selimundu.

“Tayari kampuni ya Medomix imeanza kusambaza nchini kifaa hiki baada ya kupewa kibali kutoka Wizara ya Afya,” amesema.

-->