Hifadhi Ngorongoro yasema watu wanaotaka majina yao wapewe wanyamapori kulipia

Mhifadhi mkuu wa mamlaka hiyo, Dk Fredy Manongi

Muktasari:

  • Akizungumza jana Januari 22, mwaka 2018 na wajumbe wa kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii waliotembelea hifadhi hiyo, mhifadhi mkuu wa mamlaka hiyo, Dk Fredy Manongi amesema utaratibu huo utasaidia kuongeza mapato ya Ngorongoro.

Arusha. Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) inaandaa utaratibu wa kisheria utakaowawezesha watu mashuhuri  wanaotaka majina yao waitwe wanyamapori wa hifadhi hiyo, wakiwemo faru kulipia.

Akizungumza jana Januari 22, mwaka 2018 na wajumbe wa kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii waliotembelea hifadhi hiyo, mhifadhi mkuu wa mamlaka hiyo, Dk Fredy Manongi amesema utaratibu huo utasaidia kuongeza mapato ya Ngorongoro.

Dk Manongi amesema wakati utaratibu huo ukifanyika hakuna majina mapya ambayo yatatolewa.

Awali Mbunge  wa Arumeru Mashariki (Chadema) ,Joshua Nassari na Joseph Msukuma (Geita Mjini)  waliotaka kujua mchakato wa wanyamapori kupewa majina ya viongozi.

Nassari amesema amepata taarifa kwamba kuna faru anaitwa Ndugai (Job-Spika wa Bunge), kutaka kujua sababu za kupewa jina hilo.

Akitoa ufafanuzi wa jambo hilo, Manongi amesema faru huyo kuitwa Ndugai kunatokana na Spika huyo wa Bunge kuwa mhifadhi, pia alikuwa mjumbe wa bodi ya Ngorongoro kwa muda mrefu.