Watumishi ofisi ya mkuu wa mkoa kizimbani kwa kumdhalilisha mwanahabari

Muktasari:

Wanadaiwa kumuibia simu, fedha na kumpiga picha za utupu


Arusha. Watumishi wawili wa ofisi ya mkuu wa Mkoa wa Arusha wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Arumeru wakituhumiwa kwa mashtaka mawili, likiwemo la kumvua nguo na kumpiga picha za utupu mwandishi wa habari wa kujitegemea mkoani humo, Lucas Myovela.

Watumishi waliofikishwa mahakamani leo Jumatano Mei 23, 2018 ni Swalehe Mwindadi ambaye ni ofisa itifaki katika ofisi hiyo na Amina Mshana wa kitengo cha masjala.

Awali, washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo saa tatu asubuhi.

Mbele ya Hakimu wa mahakama hiyo, Patricia Kisinda, mwendesha mashtaka wa Serikali, Sabina Silayo ameieleza mahakama kuwa washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka mawili.

Amesema shtaka la kwanza ni kufanya unyang’anyi wa kutumia silaha kinyume na kifungu cha 287A cha sheria ya kanuni ya adhabu, kifungu kidogo cha 16 kilichorekebishwa mwaka 2002.

Silayo amebainisha kuwa Mei 13, 2018 katika eneo ya Sakina jijini Arusha, washtakiwa hao kwa pamoja walimuimbia Myovela simu mbili za mkononi na Sh75,000.

Amesema katika kosa hilo, washtakiwa hao kwa pamoja walihamisha Sh9,500 kwa njia ya mtandao wa simu kabla ya kutekeleza jambo hilo wakitumia panga na mkanda wa plastiki kumtishia mwandishi huyo.

Mwendesha mashtaka amesema katika shtaka la pili, watuhumiwa walifanya ukatili na udhalilishaji kinyume na kifungu cha 138 A cha sheria ya kanuni za adhabu, kifungu kidogo cha 16 kilichorekebishwa mwaka 2002.

Amesema siku hiyo katika eneo hilohilo washtakiwa hao walimvua nguo Myovela na kisha kumpiga picha za utupu.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo, washtakiwa hao walikana na Silayo kuomba tarehe ya kutajwa kesi hiyo kwa kuwa upepelezi bado haujakamilika.

Hata hivyo, Hakimu Kisinda aliamuru washtakiwa hao kupelekwa mahabusu katika Gereza Kuu la Kisongo kwa kuwa kosa la kwanza linalowakabili halina dhamana na kuahirisha kesi hiyo hadi Juni 6, 2018.