Waumini waingia kanisani na mabango kumpinga Askofu

Waumini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kusini Mashariki wakiwa na mabango walipohudhuria ibada kwenye Kanisa Kuu la Mtwara jana. Picha na Haika Kimaro

Muktasari:

  • Wamlalamikia askofu kwa madai ya ukiukaji katiba, mwenyewe azungumza

Mtwara. Waumimi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), Dayosisi ya Kusini Mashariki, Kanisa Kuu la Mtwara wameingia katika ibada na mabango yaliyokuwa na ujumbe mbalimbali wa kumpinga Askofu Mkuu wa dayosisi hiyo, Lucas Mbedule kwa tuhuma za kukiuka katiba, unyanyasaji wa watumishi na ubadhirifu wa fedha za ushirika na dayosisi.

Hata hivyo, Askofu Mbedule amesema asingependa kuyazungumzia suala hilo kwa sababu walikaa kikao.  

Umoja  wa wazee ulitoa tamko ndani ya kanisa hilo kutokana na tuhuma zinazomkabili askofu huyo na kumtaka asijihusishe na mambo yanayohusu usharika na dayosisi, ili kupisha uchunguzi na kumwomba Mkuu wa KKKT, Dk Fredrick Shoo kuunda tume kuchunguza tuhuma hizo.

Akisoma tamko la wazee wa kanisa hilo, Amon Mkocha amesema wanapinga uamuzi uliofanywa na kikao cha halmashauri kuu kilichofanyika mwezi huu.