Wawekezaji wa ndani watakiwa kuwa chachu

Muktasari:

Hayo yalielezwa na Mkurugenzi wa Kiwanda cha NMC, Phillemon Mollel maarufu Monaban alipowasilisha taarifa ya kiwanda hicho kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa. Mollel alisema wanafurahishwa na hatua ya Serikali ya ufufuaji na uendelezaji viwanda nchini, lakini inaweza kutimia iwapo wazawa watapewa kipaumbele na kuungwa mkono.

Arusha. Serikali imetakiwa kutumia wawekezaji wa ndani ili kutimiza kampeni yake ya kuwa nchi ya viwanda, itakayopunguza tatizo la ajira kwa vijana.

Hayo yalielezwa na Mkurugenzi wa Kiwanda cha NMC, Phillemon Mollel maarufu Monaban alipowasilisha taarifa ya kiwanda hicho kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa. Mollel alisema wanafurahishwa na hatua ya Serikali ya ufufuaji na uendelezaji viwanda nchini, lakini inaweza kutimia iwapo wazawa watapewa kipaumbele na kuungwa mkono.

“Sera hii ni nzuri lakini ili izae matunda lazima Serikali itoe kipaumbele kwa wazawa, lengo likiwa ni kuhahakisha ajira zinapatikana kwa vijana, kutumia malighafi za wakulima wetu na kulipa kodi,” alisema.

“Mfano mzuri ni mimi niliyekodishwa kiwanda hiki tangu mwaka 2007 kikiwa chakavu, lakini nimekifufua na kuboresha mashine za kusaga. Pia, nimepanua kiwanda kwa kuongeza mashine za kukamua mafuta ya alizeti, kusaga ngano na kutengeneza mikate,” alisema.

Majaliwa alisema siri ya Serikali kuhamasisha nchi ya viwanda ni kupunguza tatizo la ajira nchini, kuongeza mapato na kuwapatia wakulima soko la mazao yao.

Awali, Majaliwa alitembelea kiwanda cha kutengeneza magari ya utalii na malori ya taka.