Friday, August 10, 2018

Wazazi watupwa jela siku 28 kwa kupakiza watoto kwenye bodaboda

 

By Herieth Makwetta, Mwananchi hmakweta@mwananchi.co.tz

Tanga. Upo mkoani Tanga na unataka kumuwahisha mtoto wako shule kwa kutumia usafiri wa bodaboda? Katika hili yakupasa uwe makini kwani kama mwanao ana umri wa chini ya miaka tisa unaweza kuingia matatani.

Kama huamini, basi tambua kuwa kwa kipindi cha siku 30 wazazi saba wamekamatwa, kufikishwa mahakamani na kuhukumiwa kifungo cha siku 28 gerezani kwa kosa hilo.

Akizungumza na Mwananchi, Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani mkoani hapa (RTO), Solomon Mwangamilo alisema jana kuwa wahusika walitumia usafiri wa bodaboda kuwapeleka wanafunzi shule, huku zikiwapakia zaidi ya mmoja ikiwa ni kinyume cha sheria ya leseni za usafirishaji.

Pia, watu wengine 23 wamefungwa kifungo cha siku 28 kwa kutovaa kofia ngumu (helmet) wakati wakisafiri kwa pikipiki hizo.

Mwangamilo alisema operesheni ya mwezi mmoja waliyoifanya imesaidia kurudisha nidhamu ya utii wa sheria bila shuruti.

“Watu 23 wapo jela. (Tumekuwa) tunachukua hatua ya kuwaandikia faini, kesho wanarudia kosa lilelile, kwa hiyo tukakubaliana na wenzetu tukaanza kuwafikisha mahakamani,” alisema.

Alisema adhabu ya kifungo imeleta matokeo chanya, jambo linalomfanya kila abiria na dereva wake kuvaa kofia ngumu wakati wote.

“Nia ni kuhakikisha kwamba kila mmoja anavaa kofia ngumu, mtu akivunjika mfupa au mguu atatibiwa lakini akiumia kichwa inakuwa ni shida,” alisema Mwangamilo.

Alisema faini zinazotozwa hazisaidii na hivyo waliamua kuchukua hatua kali zaidi.

“Faini wanalipa kwa sababu utamwandikia Sh30,000 atalipa, hiyo ni hela ndogo kwake haimrudishi kwenye mstari. Tunatoa adhabu kali ambayo itampa fundisho,” alisisitiza.

Pamoja na faini hizo na kifungo, kamanda huyo alisema kuna watu wengi wamefungwa kifungo cha nje na wanakwenda kila siku kufanya usafi kwenye ofisi za Serikali kwa kadri wanavyopangiwa na Mahakama. “Tunapowashughulikia wachache, hao ndiyo wanakuwa mabalozi wa wengine,” alisema.

Kuhusu wazazi wanaotumia usafiri huo kwa watoto chini ya miaka tisa, alisema bado operesheni inaendelea.

“Kila siku lazima tuwavune, hili limeanza pia kupungua hapa Tanga. (Ni vyema wananchi) tuangalie namna nyingine ya kuwapeleka watoto shule, siyo wanapanda pikipiki hawajavalishwa kofia, hiyo ni hatari kwao,” alisema.

Mkazi wa Chumbageni, Amina Salum alisema kuna baadhi ya wazazi huwapakiza bodaboda watoto wao wadogo bila tahadhari.

“Pikipiki zimekuwa kama school bus (mabasi ya shule), madereva wanawachukua wanafunzi kuwapeleka shuleni, lakini wanapakiza watoto hadi wanne, mtoto mdogo wa chekechea anakaa kwenye tenki,” alisema Amina.

Dereva wa bodaboda, Omary Kundi alisema licha ya umuhimu wa kuvaa kofia ngumu, baadhi ya abiria hususan wageni ni wabishi kuzivaa.

-->