Wazee watano na simulizi ya kusubiri kunyongwa

WAZEE WATANO NA SIMULIZI YA KUSUBIRI KUNYONGWA

Muktasari:

Magaigwa ni kati ya wazee watano walioruhusiwa kutoka Gereza Kuu la Mwanza baada ya kusubiri kutekelezwa kwa adhabu ya kunyongwa kwa miaka kadhaa, lakini wakanufaika na msamaha usio wa kawaida wa Rais John Magufuli alioutoa wakati wa maadhimisho ya miaka 56 ya Uhuru wa Tanganyika.

 Mwanza. Kwa miaka 32, Magaigwa Mahiri, mwenye umri wa miaka 70, alikuwa akiishi kwa kusubiri siku ya kunyongwa baada ya kupatikana na hatia ya kuua, lakini Desemba 9 ilirudisha matumaini mapya.

Magaigwa ni kati ya wazee watano walioruhusiwa kutoka Gereza Kuu la Mwanza baada ya kusubiri kutekelezwa kwa adhabu ya kunyongwa kwa miaka kadhaa, lakini wakanufaika na msamaha usio wa kawaida wa Rais John Magufuli alioutoa wakati wa maadhimisho ya miaka 56 ya Uhuru wa Tanganyika.

Tangu mwaka 1985, Magaigwa amekuwa akiishi bila ya kujua ‘kesho yake’, bila ya matumaini na kujiona asiye na thamani, huku jambo moja tu alilokuwa na uhakika nalo ni “siku moja atanyongwa”.

“Kukaa magereza kusubiri siku ya kunyongwa ni maisha yasiyo na matumaini na yanayokufanya kujihisi kukosa thamani machoni mwa jamii,” anasema Magaigwa, ambaye alinufaika na msamaha wa Rais John Magufuli alioutoa siku hiyo ya maadhimisho ya miaka 56 ya uhuru wa Tanganyika aliposamehe watu 61 waliohukumiwa kunyongwa.

Magaigwa anasema maisha hayo yalimfanya amgeukie Mungu kama njia pekee ya tumaini la maisha mengine baada ya kifo alichokuwa akisubiri.

“Nina miaka 32 gerezani tangu nilipokamatwa mwaka 1985 na kushtakiwa kwa kosa la mauaji. Tangu wakati huo, nimeishi bila kujua hatima yangu,” anasema.

Mzee huyo alikaa mahabusu kwa miaka mitatu wakati shauri lake likisikilizwa kabla ya kuhukumiwa kifo mwaka 1988 baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kumuua mgoni wake aliyemkuta mkewe.

Wakati wa tukio hilo, Magaigwa, ambaye ni mkazi wa Kata ya Rweng’abure wilaya ya Serengeti mkoani Mara, alikuwa na umri wa miaka 38 kulingana na hesabu za kukaa mahabusu miaka mitatu na gerezani miaka 29.

Kabla ya kukamatwa, kushtakiwa na hatimaye kuhukumiwa kifo, Magaigwa alikuwa amefanikiwa kupata watoto watano aliozaa na mkewe, Maria Wansato.

Mwingine aliyenusurika kifo ni Shija Lugeko, mwenye umri wa miaka 71 na ambaye ni mkazi wa kijiji cha Mwamwajungu wilayani Shinyanga. Alikuwa amehukumiwa kunyongwa mwaka 1999, lakini msamaha wa Rais umempa matumaini mapya.

“Niliumia kisaikolojia na kukosa tumaini la kuendelea kuishi tangu siku niliposomewa hukumu ya kunyongwa hadi kufa,” anasema Mzee Lugeko ambaye anaendelea kuishi eneo la Gereza la Butimba kwa kuwa aliwasiliana na familia yake mara ya mwisho mwaka 2000.

Kabla ya hukumu ya kifo, Lugeko alioa mwanamke anayemkumbuka kwa jina la Agnes Shija na kufanikiwa kupata watoto wawili.

Mwingine aliyemgeukia Mungu na kuwa mchungaji akiwa gerezani ni Benjamin Wandwi (67), mkazi wa kijiji cha Ngamani wilayani Serengeti aliyehukumiwa kifo mwaka 1990.

Wandwi, baba wa watoto wanne aliowapata kwa mkewe Angelina Benjamin, amesema ataendeleza imani yake.

“Nikiwa gerezani niliokoka na kuwa mchungaji huku nikiwahubiria habari njema wafungwa wenzangu pamoja na mahabusu. Hata sasa baada ya kuachiwa huru, nitaendeleza kazi ya kuhubiri Injili kuiasa na kuionya jamii dhidi ya maovu na kumrejea Mungu,” alisema Wandwi

Wengine walioachiwa huru jana kutoka Gereza la Butimba ni Chananja Luchagula (77), mkazi wa kijiji cha Busaka, Chato mkoani Geita na Maregesi Kihimba (78), mkazi wa wa wilaya ya Musoma.

Luchagula aliyeugua ugonjwa wa moyo akiwa gerezani, alihukumiwa mwaka 1988.

Kwa upande wake, Maregesi alisema taarifa za vifo vya ndugu zake watano pamoja na mkewe, Nyambaya Msaye alizozipata akiwa gerezani, zilimwongezea maumivu moyoni na kumfanya kukosa tumaini ya maisha.

“Kukaa gerezani ukisubiri kunyongwa ni adhabu kuliko hata kunyongwa kwenyewe kwa sababu unaishi bila kujua kesho yako,” anasema Maregesi ambaye alikaa gerezani kwa miaka 17.

Kivutio wakati wakiachiwa

Kama kuna mtu aliyekuwa na furaha iliyopitiliza jana wakati watu hao wakiachiwa huru, basi ni ‘Mchungaji’ Benjamin Wandwi ambaye alimkuta langoni mtoto wake, Zablon Benjamin (28), ambaye alikuwa na miaka mitatu wakati akihukumiwa.

Baba na mwanae, ambaye alikuwa akimtembelea mzazi wake mara kwa mara, walikumbatiana kwa furaha huku kila mmoja akibubujikwa machozi ya furaha.

“Nimekuwa na maisha magumu ya kuishi bila baba nyumbani, kila wakati nilikuwa nafika gerezani kumsalimia,” alisema Zablon huku akilengwa machozi ya furaha

Kutokana na kukosa malezi na matunzo ya baba, Zablon alisema alishindwa kuendelea na elimu ya sekondari licha ya kufaulu mtihani wa darasa la saba.