Waziri Mkuu India ampiku Magufuli

Muktasari:

Akizungumza katika mkutano wa 14 wa mwaka wa wahandisi uliofanyika Septemba Mosi katika Ukumbi wa Mlimani City, Rais Magufuli alisema kwa mamlaka aliyonayo anaweza kuamua kubadili fedha ili zile zinazofichwa, watu hao wakose mahali pa kuzipeleka.

New Delhi/ Dar es Salaam. Wakati Rais John Magufuli alitishia kubadili fedha za Tanzania katika juhudi za kuwadhibiti watu wanaodaiwa kuficha fedha, Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi ametangaza kuziondoa kwenye mzunguko noti za Rupia 500 na 1,000.

Akizungumza katika mkutano wa 14 wa mwaka wa wahandisi uliofanyika Septemba Mosi katika Ukumbi wa Mlimani City, Rais Magufuli alisema kwa mamlaka aliyonayo anaweza kuamua kubadili fedha ili zile zinazofichwa, watu hao wakose mahali pa kuzipeleka.

Alisisitiza kwa kusema kauli hiyo ni mahsusi kwa watu walioficha fedha katika majumba yao na kuwataka kuacha tabia hiyo mara moja ili fedha hizo ziingie katika mzunguko.

Rais Magufuli alisema katika utawala wake fedha za bure hazitakuwapo kwa sababu zilizokuwapo awali zilitokana na fedha za wizi kutoka serikalini ambazo kwa sasa zimedhibitiwa.

Alisema kwa mwendo anaokwenda nao sasa ni ngumu kwa mwananchi kupata fedha bila kufanya kazi.

Habari kutoka India zinasema Waziri Mkuu Modi alitangaza hatua hiyo ya kushangaza kwenye runinga Jumanne usiku kuwa ni mojawapo ya harakati za kukabiliana na ufisadi na ukopeshaji wa fedha haramu.

Modi alisema noti zote za Rupia 500 na 1,000 “hazitakuwa fedha halali kuanzia usiku wa manane leo” na kwamba “zitabaki kuwa makaratasi yasiyo na maana.” Hata hivyo, alisema noti nyingine za Rupia 100, Rupia 50, Rupia 20, Rupia 10, Rupia 5, Rupia 2 na sarafu zote zitaendelea kuwa na thamani.

“Ulanguzi wa fedha na ufisadi ndiyo vikwazo vikuu katika kukabiliana na umasikini,” alisema Modi na kuongeza: “Watu wataweza kubadilisha noti zao za zamani na mpya katika benki kuanzia Novemba 10 hadi Desemba 30 na kwamba fedha hizo hazitatumika tena.”

Benki zilifungwa jana huku huduma za mashine za kutoa pesa za ATM zikisitishwa. Badala yake noti mpya za Rupia 500 na 2,000 zitawekwa katika mfumo wa fedha kuchukua nafasi ya zilizoondolewa.

Tangazo hilo lilisababisha mtafaruku kwenye vituo vya mafuta na maeneo mengine ya biashara kwani wauzaji wa rejareja walikuwa wakikataa kupokea noti hizo huku mashine za kutolea fedha zikifungwa. Katika viwango vya ubadilishaji fedha noti ya Rupia 500 ni sawa na Sh16,000 na Rupia 1,000 ni sawa na Sh32,000.

Wateja watakuwa na uwezo wa kubadili noti hizo ili wapewe mpya au kuziweka kwenye akaunti, lakini watatakiwa kujieleza mamlaka ya mapato walivyozipata.