Waziri Mkuu kuongoza mazishi waliofariki dunia kwenye kivuko

Muktasari:

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa atawasili kijiji cha Bwisya Kisiwa cha Ukara kushiriki ibada ya mazishi ya watu waliofariki dunia katika ajali ya kivuko cha MV Nyerere

Ukerewe. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa natarajiwa kuwasili katika kijiji cha Bwisya Kisiwa cha Ukara kuongoza ibada ya mazishi ya baadhi ya watu waliopoteza maisha katika ajali ya Kivuko cha MV Nyerere iliyozama Septemba 20, 2018.

Akizungumza leo Jumapili Septemba 23, 2018 mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella amesema kiongozi huyo atajumuika na viongozi wengine ambao wapo kisiwani hapa kushiriki mazishi  ya miili ambayo haijatambulika na ambayo ndugu wameomba izikwe kwa utaratibu ulioandaliwa na Serikali.

Zaidi ya miili 225 imeopolewa, miili 172 kutambuliwa na 112 imechukuliwa na ndugu kwa ajili ya mazishi huku 37 ikiwa haijatambuliwa hadi leo asubuhi.

Kila mwili unaotambuliwa na kuchukuliwa na ndugu, familia hukabidhiwa ubani wa Sh500,000 na Serikali, jeneza na usafiri wa kivuko au meli hadi ghati la Bugolora.