Waziri Mpango: Aibu kuomba misaada nje ya nchi

Muktasari:

Dk Mpango alisema hayo jana alipofunga mafunzo ya wadadisi, wasimamizi na wahariri wa takwimu za mapato na matumizi binafsi katika ngazi ya kaya.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango amesema amechoka kuomba misaada nchi za nje kwa sababu ni aibu na jambo hilo linalidhalilisha Taifa.

Dk Mpango alisema hayo jana alipofunga mafunzo ya wadadisi, wasimamizi na wahariri wa takwimu za mapato na matumizi binafsi katika ngazi ya kaya.

“Misaada imekuwa ikidhalilisha Taifa, wanasema kweli sisi ni nchi ya tatu katika upatikanaji wa dhahabu halafu waziri wao wa fedha anakuja kuomba,” alisema.

Alifafanua kuwa ni lazima nchi iwe na mkakati wa kuondokana na hali hiyo na malengo yatafikiwa kama makusanyo ya takwimu yatafanyika na kutumiwa kwa weledi na umakini.

“Hamna budi kufuata sheria na kanuni za utumishi. Taarifa mtakazozipata ni za siri hamtakiwi kutoa kokote, ni kwa ajili ya matumizi ya takwimu pekee. Mkifanya vinginevyo, mahakamani,” alionya.

Dk Mpango alisema kwamba watakaovuruga kazi inayoanza mwezi huu na kumalizika baada ya miezi sita watabanwa.

“Siku za nyuma kuna watu walikwenda kukusanya takwimu wakaleta, tukaanza kuulizana kwanini idadi ya watu imepungua? Kumbe walikwenda kupika takwimu katika mikorosho, msiende kutusaliti,” alitahadharisha.

Pia, alizitaka kaya zilizochaguliwa kutoa taarifa sahihi wanapofikiwa na wadadisi wa takwimu na viongozi wa ngazi ya Taifa huko vijiji, kutoa ushirikiano kwenye maeneo yao.

Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Takwimu (NBS), Dk Albina Chuwa alisema kwamba kwa kutumia teknolojia wameweza kupunguza matumizi kutoka Sh20 bilioni hadi Sh10 bilioni, fedha zitakazokamilisha kazi hiyo.

Alisema huo ni utafiti wa saba na watahakikisha wanatoa matokeo ya awali ya utafiti katika kipindi cha miezi sita kuanzia sasa ili yafanyiwe kazi.

“Nendeni mkafanye kazi kwa uadilifu na uaminifu mkubwa bila kufanya udanganyifu, maana hatutashindwa kuchukua hatua kwa watakaobainika,” alionya.

Dk Chuwa aliongeza kwamba kaya zisizopungua 10,460 zitahusika katika utafiti huo utakaohusisha wadadisi 620.