Waziri aeleza sababu za kununua ndege Bombadier

Muktasari:

Profesa Mbarawa alitoa kauli hiyo jana wakati akizindua mafunzo ya wakufunzi ya marubani yanatolewa na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kilichopo Mabibo, Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amesema Serikali iliamua kununua ndege aina ya Bombadier Q400 kutoka Canada kutokana na uhitaji wa huduma ya usafiri wa anga kwa safari za ndani ya nchi na mazingira halisi ya viwanja vya ndege vilivyopo nchini.

Profesa Mbarawa alitoa kauli hiyo jana wakati akizindua mafunzo ya wakufunzi ya marubani yanatolewa na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kilichopo Mabibo, Dar es Salaam.

“Serikali imeamua kununua aina hii ya ndege za Bombadier Q400 kutokana na hali halisi ya viwanja vya ndege nchini kuwa vya changarawe na lami kwa baadhi,” alisema Profesa Mbarawa.

Profesa Mbarawa aliyeonekana kujibu hoja za wabunge wa Kamati ya Miundombinu walipokutana na Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) na Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA) mjini Dodoma hivi karibuni, alisema kuwa Serikali haikukurupuka kufanya uamuzi wa kununua aina hiyo ya ndege kwani ilizingatia vigezo na malengo mahsusi ya kuhudumia usafiri wa ndani na kuboresha usafiri wa anga kupitia ATCL.

Katika kikao hicho cha Kamati ya Bunge ya Miundombinu, Mbunge wa Misungwi (CCM) na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga alipinga Serikali kununua ndege hizo zinazotumia injini za pangaboi kwa fedha taslimu huku kukiwa hakuna mipango thabiti ya kuifanya ATCL iwe bora.

“Ukiangalia mikakati ya kutanua hili shirika (ATCL) liende juu hakuna, tunachozungumzia ni kununua ndege. Sasa ukishanunua zije zifanye nini? Zife na zenyewe? Ziishe kama tulivyonunua nyingine? Hivyo ndivyo tutakavyoendesha uchumi wetu, mimi naambiwa Q400 ndiyo tutakuwa watu wa kwanza kuipokea, halafu mnaifahamu hii kampuni? Si kubwa kama inavyotajwa, ni mali ya mtu binafsi,” alisema.

Lakini Profesa Mbarawa alitetea uamuzi wa kununua ndege hizo huku akiwataka Watanzania kuelewa nia ya Serikali yao ni kuhudumia wananchi, hivyo watu wasipotoshe ukweli kuhusu ndege hizo kwa kuwa zimezingatia mambo mbalimbali likiwamo suala la usalama na ufanisi katika uendeshaji wake.

Uwezo na ubora

Profesa Mbarawa alisema ndege hizo zina uwezo wa kutua katika viwanja vingi vyenye urefu wa kilomita 1.5 ambavyo ni vingi nchini tofauti na aina nyingine ambazo hutua kwenye viwanja vyenye urefu zaidi ya kilomita mbili.

Pia, zinatumia kiasi kidogo cha mafuta ikilinganishwa na aina nyingine ambapo kwa safari ya kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza zitakuwa zikitumia tani 1.7 za mafuta tofauti na aina nyingine zinazotumia hadi tani 2.8 kwa safari moja.

Vilevile, alitumia fursa hiyo kukanusha uvumi ulionezwa kuwa ndege hizo zimenunuliwa katika kampuni ndogo isiyokuwa na sifa akisema kampuni hiyo imefanya biashara na nchi nyingi ikiwamo Ethiopia yenye ndege 19 aina ya Bombadier Q400 zilizotengezwa na kampuni hiyo.

Tayari Serikali imeshafanya malipo ya ununuzi wa ndege hizo kwa asilimia 40 na zitaanza safari ya kutoka Canada Septemba 15 mwaka huu kupitia Uingereza na zinatarajiwa kuwasili nchini Septemba 19.