Waziri kukutana na maofisa wake kujadili sakata la ving’amuzi

Muktasari:

TCRA imetoa kusudio la kusimamisha leseni kutokana na madai ya kukiuka masharti.


Dar es Salaam. Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe amesema atakutana na wasaidizi wake akiwamo katibu mkuu wa wizara na mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Mawasiliano Tanzania (TCRA) kujadili kusudio la kusitisha leseni za baadhi ya kampuni zinazotoa huduma ya ving’amuzi.

Kamwelwe alisema hayo jana baada ya kutafutwa na Mwananchi kuzungumzia sintofahamu iliyoibuka na kusababisha taharuki kwa watumiaji wa ving’amuzi vya DSTV na Zuku ambavyo TCRA imetoa kusudio la kusimamisha leseni zao kutokana na madai ya kukiuka masharti.

Waziri huyo alisema ingawa ni mgeni katika wizara hiyo, lakini mtu anapokiuka matumizi sahihi ya leseni hawezi kuachwa.

Alisema kwa kuwa suala hilo limekuwa nyeti na limeibua sintofahamu anahitaji kukutana na katibu mkuu wa wizara na mkurugenzi mkuu wa TCRA kabla ya kutoa taarifa kwa umma.

“Suala hili ni yaleyale ya Wizara ya Maji, unakuta taasisi ya Serikali inadaiwa bili kubwa, lakini tukitaka kukata maji kwa mujibu wa utaratibu wananchi wanalalamika kuwa wanakosa huduma wakati si kosa lao, hivyo basi nikuombe kesho (leo) ulete maswali yako kwa maandishi ili wataalamu wizarani wayajadili na mimi nipate cha kuwaambia watu,” alisema Kamwelwe.

Kusudio la kufutwa

TCRA imesema inakusudia kusimamisha leseni za kampuni za Multichoice Tanzania wamiliki wa king’amuzi cha DSTV na Simbanet Tanzania inayomiliki Zuku kwa kukiuka masharti.

Tangazo la TCRA lililotolewa kwenye vyombo vya habari juzi, lilieleza kuwa Zuku na Dstv zimekuwa zikionyesha chaneli zilizopo kwenye orodha ya zile za bure kinyume cha matakwa ya leseni zao.

Wakati tangazo la TCRA likiwahusu Multichoice na Simbanet, king’amuzi cha Azam juzi kiliondoa kwenye orodha yake chaneli za bure.

Juhudi za kuupata uongozi wa Azam kuelezea suala hilo jana hazikuzaa matunda.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Vipindi na Utangazaji wa Clouds Media Group (CMG), Ruge Mutahaba alisema hapingani na utaratibu wa kisheria, lakini hatua ya Serikali kuondoa kwenye orodha chaneli hizo inaathiri biashara yao kwa kiasi kikubwa.

Matangazo ya Clouds TV hurushwa kupitia king’amuzi cha Azam.

“Misingi ya biashara yetu inategemea unawafikia watu wangapi, kwa sababu sisi hatuna kosa lolote taarifa ya hatua kama ile inabidi tupewe mapema ili tuwaeleze wateja wetu. Kama jana tumepotea Azam TV ghafla, tunawaambiaje watu sasa,” alisema Mutahaba.

Alisema kwa zama za sasa kila mwenye maudhui (content) anatamani yawafikie watu wengi zaidi lakini kupitia jukwaa lenye ubora.

TCRA juzi ilitoa tangazo kwa ajili ya Dstv na Zuku ikiwa ni siku chache baada ya jingine lililoeleza kusudio la kusimamisha leseni ya kampuni ya Starmedia inayomiliki king’amuzi cha Startimes kwa madai ya kukiuka masharti.

Maelezo ya TCRA

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa TCRA, Semu Mwakyanjala alipotafutwa na Mwananchi kutoa ufafanuzi juzi, alisema lengo la mamlaka si kuadhibu bali kuzingatia utaratibu wa kisheria.

Alisema watoa huduma hao walishaambiwa muda mrefu lakini hawazingatii maelekezo. “Watoa huduma hupewa utaratibu wanapopewa leseni na kinachofanyika sasa wanakifanya kwa makusudi,” alisema.

Aliongeza kuwa, “kwa kawaida tukitoa notisi kama hivi hatua huwa zinachukuliwa baada ya siku 30, lakini hapa kati mtu akifuata utaratibu wa leseni anaendelea na huduma kama kawaida.” Hata hivyo, Ofisa Habari wa Multichoice Tanzania, Johnson Mshana alisema kuna shauri katika Tume ya Ushindani kuhusu jambo lililosababisha TCRA kuwapa notisi.