Friday, October 13, 2017

Weah aongoza Liberia, marudio yanukia

 

Monrovia, Liberia. Matokeo rasmi ya awali ya urais yaliyotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) yanaonyesha Seneta George Weah wa chama cha upinzani cha CDC anaongoza kwa tofauti ya kura 31,150 dhidi ya mpinzani wake wa karibu Joseph Boakai wa UP.

Mashabiki wa UP ambacho ni chama tawala huenda wakapata mshtuko mkubwa kutokana na CDC kuongoza katika maeneo kadhaa ambayo yalikuwa ngome ya Unity Party (UP). Zaidi ya watu 2.1 milioni walijiandikisha kupiga kura.

Kwa mujibu wa matokeo hayo ya awali yaliyotangazwa na NEC hadi Alhamisi jioni, jumla ya kura halali ni 349,357 kati ya 371,378. Kura batili ni 22,021 sawa na asilimia 5.93. Kati ya kura hizo CDC imenyakua kura 137,606 sawa na asilimia 39.39, UP kura 106,456 sawa na asilimia 30.47 na wagombea wengine 18 wameambulia kura 105,295 sawa na asilimia 30.14.

Mshindi katika kinyang'anyiro hicho anapaswa kujipatia asilimia 50 jumlisha moja ya kura zote ili aweze kutangazwa mshindi na ikiwa mwelekeo wa ushindani utaendelea kuwa hivi upo uwezekano wa Weah na Boakai kupambana katika duru ya pili mwezi ujao kuamua mshindi.

Wagombea 20 akiwemo mwanamke mmoja wamejitokeza kuwania kumrithi mwanamke wa kwanza Afrika kuwa rais Ellen Johnson Sirleaf anayemaliza muda wake kwa mujibu wa katiba ya taifa. Mshindi huyo wa Tuzo ya Nobel ameongoza mihula miwili ya miaka sita sita.

NEC imesema kwamba itaendelea kutangaza matokeo ya vituo 4,158 vilivyosalia kadri inavyokamilisha ukokotoaji.

 

-->