Wema Sepetu atoa sababu za kuhamia Chadema

Muktasari:

Wema alitangaza kuhamia Chadema jana alipofanya mkutano na waandishi wa habari, akiwa pamoja na mama yake, meya wa Ubungo na mashabiki wake, maarufu kama “Team Wema” waliovalia sare za rangi za chama hicho kikuu cha upinzani na ambao walikuwa wakimpigia makofi kila alipozungumza.

Dar es Salaam. Msanii maarufu nchini, Wema Sepetu amesema uamuzi wake wa kuihama CCM na kujiunga Chadema, hautokani na sakata lake dhidi ya vyombo vya dola, lakini akaeleza mlolongo wa matukio yaliyomtokea yeye, wasanii wenzake na chama hicho tawala.

Wema alitangaza kuhamia Chadema jana alipofanya mkutano na waandishi wa habari, akiwa pamoja na mama yake, meya wa Ubungo na mashabiki wake, maarufu kama “Team Wema” waliovalia sare za rangi za chama hicho kikuu cha upinzani na ambao walikuwa wakimpigia makofi kila alipozungumza.

Wema amefunguliwa mashtaka ya kutumia dawa za kulevya kwa madai kuwa alikutwa na msokoto wa bangi baada ya mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kumtaka aripoti kituo kikuu cha polisi jijini Dar es Salaam kwa mahojiano na baadaye kwenda kupekuliwa nyumbani kwake. Ilikuwa ni baada ya kushikiliwa kituoni kwa siku tatu.

“Kama ni kuhama ingekuwa wakati ule nilipokatwa jina nilipogombea ubunge,” alisema Wema ambaye aligombea ubunge wa viti maalumu kwa tiketi ya chama hicho akipitia mkoa wa Singida.

“Nililia chumbani, lakini sikujivua uanachama wa CCM.”

Baada ya kukatwa, binti huyo wa Balozi Isaack Sepetu pamoja na wasanii wenzake walizunguka nchi nzima wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 2015, wakimnadi mgombea mwenza wa urais kwa tiketi ya CCM, Samia Suluhu wakiwa na kauli mbiu ya “Mama Ongea na Mwanao”.

Wakati Wema akizunguka kuinadi CCM katika uchaguzi huo uliokuwa na upinzani mkali, wasanii wengine walipanda jukwaa la mgombea urais wa chama hicho, John Magufuli na wengine kwa mgombea wa Chadema na Ukawa, Edward Lowassa.

Lakini Wema, ambaye juzi alimsindikiza mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe mahakamani, jana alisema ameyaweka hayo kando, na sasa amevaa “gwanda kupigania demokrasia waliyoizoea”.

Akijibu maswali ya waandishi wa habari, likiwemo la sababu za kuondoka chama alichokipigia kampeni nchi nzima akiwa na wasanii wenzake, Wema alisema uamuzi wake hautokani na madena ambayo wanaidai CCM.

Ingawa alisema hayupo tayari kuzungumzia kwa kina kiwango cha fedha ambacho wsanii wanakidai chama hicho, Wema alisema wamekuwa wakizungushwa malipo yao.

“Siwezi kusema ni kiasi gani kwa sasa, lakini tambua kwamba ni kweli tunadai na tumekuwa tuikijibiwa kwamba tumfuate (Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete) JK tukamdai hayo madeni yetu,” alisema Wema kwenye mkutano wake huo uliokuwa unafanyikia nyumbani kwao Sinza-Kijitonyama na kurushwa moja kwa moja na mitandao ya kijamii.

Hata hivyo, naibu katibu mkuu wa CCM upande wa Bara, Rodrick Mpogolo alikataa kusema lolote kuhusu madai hayo, akisema yeye si mlipaji na si msanii kiasi cha kujua ni kina nani hawajalipwa.

“Ushauri wangu waende kwa mlipaji au mhusika wa mchakato huu kama kweli hawajalipwa, si kukimbilia kwenye vyombo vya habari. Mhusika wanamjua na wala si JK ambaye alikuwa mwenyekiti tu CCM,” alisema Mpogolo.

Naye naibu katibu mkuu wa chama hicho upande wa Zanzibar, Vuai Ali Vuai alikuwa na maoni kama ya Mpogolo, akisema halifahamu suala hilo na hana taarifa.

Alisema kama kweli wasanii hao ni haki yao, waende kwa mtu aliyewapa kazi hiyo.

“CCM ni chama kikubwa na kina vitengo vingi hivyo ni vyema wakaenda kwa mhusika ili kupewa utaratibu wa malipo ya madai yao,” alisema Vuai.

Mbali na madai ya fedha kutokana na kampeni, Wema pia alisema chama hicho tawala kimemtelekeza katika matatizo yake ya sasa na vyombo vya dola.

Mshindi huyo wa taji la Miss Tanzania mwaka 2006, alisema ameshangaa jinsi viongozi wa CCM walivyoshindwa kuwa karibu naye. Alidai kuwa hata wasanii wenzake hawajitokezi kwa kuwa wametishwa na hivyo kumtenga.

“Hali hii imenifanya nijisikie mnyonge licha ya kufanya juhudi wakati wa kampeni,” alisema muigizaji huyo maarufu wa filamu aliyechomoza na sinema ya Point of No Return.

Alisema alijitolea kwa utu wake kushiriki kikamilifu katika shughuli za CCM, huku akikumbuka jinsi alivyowahi kuahidi kuwa angekufa akiwa kwenye chama hicho, lakini hakujua kama yangetokea haya ya sasa.

Alisema alirithi ufuasi wa CCM kwa baba yake, ambaye amewahi kuongoza wizara tofauti katika serikali za awamu zilizopita na pia Serikali ya Mapinduzi, ikiwamo uwaziri na kuwa mshauri wa Rais wa Zanzibar.  

“Hadi anakufa baba alikuwa ni kada wa CCM, nami ndiye nilipokea ukada kutoka kwake. Niliahidi ningefia CCM, lakini natamani ningejua mapema. Ndiyo hivyo ya Mungu ni mengi,” alisema Wema.

“Kweli tenda wema nenda zako, usingoje shukrani.”

Kuhusu kesi yake, Wema alisema: “Dola ibaki ifanye kazi yake kama dola, wala sipo hapa kuikataza, lakini iangalie haki za binadamu.”

Wema alisema anaamini kuwa uamuzi alioufanya ni sahihi, kwa kuwa alijiuliza maswali ya kutosha kwamba ni wapi alipoikosea CCM hadi kufikia hatua ya kumnyong’onyeza.

“Isichukuliwe kwamba nimefanya uamuzi huu kwa hasira. Uamuzi wangu ni sahihi. Nimeingia katika vita nimevaa magwanda. Nipo tayari kupigana, nina imani kwamba kuna watu wapo nyuma yangu watanifuata,” alisema.

Wema, ambaye alikuwa akizungumza hayo huku akiwa na mlinzi nyuma yake, alisema ameamua kujiunga Chadema kwa sababui ni chama ambacho kilikuwa kinaisumbua CCM wakati wa kampeni kutokana na kujinadi kuwa kinapigania demokrasia ambayo alisema inaonekana.

“Sijachukua wala kulipwa chochote na Chadema. Kama nimepewa pesa, kaburi la baba yangu kule Zanzibar lipasuke katikati,” alisema Wema akizungumzia baba yake ambaye alizikwa Zanzibar.

“Huu si wakati wa kampeni nimeamua kwa kuwa nimehisi kwamba nchi yetu inaenda kupoteza demokrasia ile ambayo tuliizoea. Sasa nimejiunga huku ili kuisaka hatmaye ndani ya nguvu ya wananchi tuigeuze nchi yetu iwe kama tunavyotaka,” alisema Wema.  

Akizungumza katika mkutano huo, mama yake Wema alisema bintiye amedhalilishwa na kuteswa, jambo ambalo ameshindwa kuvumilia kwa sababu anatambua mchango wake yeye kama mwenyekiti wa CCM wa Tawi la Nzasa lililopo Kata ya Kijitonyama.

“Mwanangu hawezi kuteswa huku CCM inaangalia na mbaya zaidi hakuna hata mwanaCCM aliyejitokeza kumjulia hali. Nina watu 5,000 watanifuata hadi watu wa ukoo wangu. Baba wakati anakufa alituacha tupo 72, sasa tumeongezeka wote hao wamesema wanahama huko,” alisema mama huyo.

Wema na mama yake walikabidhi kadi hizo kwa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chadema, Boniface Jacob , ambaye pia ni Meya wa Halmashauri ya Ubungo.

Jacob alieleza kufurahishwa na hatua ya Wema kujiunga Chadema akisema itaongeza nguvu kwa vijana ndani ya chama hicho.

“Wema ameamua kuingia Chadema ili kujiunga nasi. Tunafurahi, tunajua kwamba ana watu wengi, na atashiriki katika kukiongezea ushindi chama. Huyu amechukua uamuzi huu katika wakati ambao si wa kampeni, ameonyesha jinsi alivyojitoa,” alisema.

Alisema amepokea kadi za CCM zilizorudishwa na mwenyekiti wa Chadema atawakabidhi rasmi kadi za kujiunga na chama hicho.

Nyongeza na Bakari Kiango