Wizara ya Fedha yashinda tuzo

Waziri wa Fedha, Philip Mpango.

Muktasari:

Tuzo hizo zilitolewa jana na Kamishna Msaidizi Sera, wa Wizara ya Fedha, Shogholo Msangi kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dotto James.

Dar es Salaam. Wizara ya Fedha na Mipango, imepata tuzo ya kuandaa vitabu bora vya mahesabu vinavyokidhi viwango vilivyowekwa na Bodi ya Taifa ya Uhasibu na Ukaguzi (NBAA).

Tuzo hizo zilitolewa jana na Kamishna Msaidizi Sera, wa Wizara ya Fedha, Shogholo Msangi kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dotto James.

Msangi alisema aliwataka wahasibu nchini kuzingatia viwango vya uhasibu vinavyotakiwa na kukubalika kitaifa na kimataifa wakati wa kuandaa taarifa za fedha.

Akizungumza katika tukio hilo ambalo liliambatana na kufungwa kwa Mkutano wa mwaka wa Wahasibu unaojumuisha nchi za Afrika Mashariki, Msangi alisema:

“Taarifa za fedha hutumika katika matumizi mbalimbali katika Sekta ya umma na binafsi, hivyo iwapo taarifa hizo zitakuwa katika viwango vyenye ubora zitaongeza imani ya wananchi kwa Serikali yao,” alisema

Amesema kuwa taarifa hizo pia hutegemewa na wawekezaji katika kupanga maamuzi yao ya uwekezaji hapa nchini hatua itakayosaidia nchi kufikia malengo yake ya kuwa nchi ya viwanda na uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.