Zanu PF wafikiria kumuondelea kinga Mugabe, kumnyima marupurupu

Muktasari:

Mangwana alisema rais huyo wa zamani anapaswa kuwa "Baba wa Taifa" na "haipaswi kujiunga na siasa za harakati, zinazofahamika kama za upinzani".


Harare, Zimbabwe. Chama tawala cha Zanu PF kimesema Robert Mugabe anaweza kupoteza kinga ya kutoshtakiwa pamoja na marupurupu kama mkuu wa zamani wa nchi ikiwa pamoja na kufukuzwa kwenye chama.

Haya yamekuja baada ya Mugabe wiki iliyopita kuwaambia waandishi wa habari kwamba Rais Emmerson Mnangagwa amewekwa madarakani na jeshi na hivyo anatawala kinyume cha sheria.

"Zanu-PF itatakiwa kukutana ili kujadili maendeleo haya mapya ... kupitia upya kama bado ni muhimu au la kwake (Mugabe) kuendelea kufurahia heshima tuliyompa," katibu wa masuala ya kisheria katika chama, Paul Mangwana aliliambia gazeti la serikali la Herald.

Mbali na maoni yake kwa waandishi wa habari wa kimataifa Alhamisi iliyopita, Mugabe pia alikosolewa kwa hatua yake ya kufanya mkutano wiki mbili zilizopita na waziri wa zamani, Ambrose Mutinhiri, ambaye sasa anaongoza chama cha upinzani cha National Patriotic Front (NPF).