Serikali yaweka hadharani yaliyozungumzwa ziara ya viongozi wa Oman

Muktasari:

  • Oman itatoa msaada wa kiufundi na kisheria katika sekta ya mafuta na gesi kila inapohitajika kufanya hivyo.

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imezungumzia ujio wa viongozi kutoka nchini Oman waliotumia meli ya Sultan Qabous yenye jina la Fulk Al Salam kwamba haukuwa wa kisiasa.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Ikulu, Issa Haji Ussi ‘Gavu’ amesema hayo leo Jumapili Oktoba 22,2017 alipotoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu ziara ya viongozi hao.

Amesema lengo la ujumbe huo kutoka nchini Oman uliofika Zanzibar wiki iliyopita lilikuwa kueneza amani, kukuza ushirikiano na uhusiano uliopo kati yao na Zanzibar na kubadilisha mawazo juu ya kufikisha maendeleo kwa jamii.
Gavu amesema katika kipindi chote cha siku nne cha uwepo wa ujumbe huo Zanzibar, ulikutana na viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kuzungumzia uhusiano uliopo na ushirikiano katika kuimarisha sekta za utalii, viwanda, elimu, uwekezaji, mafuta na gesi.

Amesema miongoni mwa mambo waliyokubaliana kati ya Serikali ya Oman na SMZ ni matengenezo ya jengo la Beit-el-Ajab, ukarabati wa jengo la People’s Palace’ na uwekezaji katika viwanda vya kusindika samaki na kutengenezea juisi.

Makubaliano mengine amesema ni kuitangaza Zanzibar kiutalii na kuanzisha safari za moja kwa moja za watalii kati ya Zanzibar na Oman.

Pia, kutoa msaada wa kiufundi na kisheria katika sekta ya mafuta na gesi kila inapohitajika kufanya hivyo na kutoa mafunzo ya muda mfupi na mrefu katika masuala ya mafuta na gesi asilia.

Mshauri wa Rais, Balozi Mohammed Ramia amesema Zanzibar imepata heshima kubwa kwa kuwa na uhusiano mzuri na nchi za nje ambazo viongozi wake wamekuwa wakifanya ziara visiwani humo