Zitto ahoji Bunge kutogharamia matibabu ya Tundu Lissu

Muktasari:

Lissu ambaye ni mbunge huyo wa Singida Mashariki, alishambuliwa kwa risasi zaidi ya 30, Septemba 7, mwaka jana na kupelekwa Hospitali ya Rufaa ya Dodoma na siku hiyohiyo kuhamishiwa Hospitali ya Nairobi ambako alilazwa hadi Januari 6 alipohamishiwa Ubelgiji anakoendelea na matibabu hasa mazoezi ya viungo.

 Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT Wazalendo), Zitto Kabwe amemtembelea Tundu Lissu anayepatiwa matibabu katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha Leuven nchini Ubelgiji na kuhoji sababu za Bunge kutogharamia matibabu yake.

Lissu ambaye ni mbunge huyo wa Singida Mashariki, alishambuliwa kwa risasi zaidi ya 30, Septemba 7, mwaka jana na kupelekwa Hospitali ya Rufaa ya Dodoma na siku hiyohiyo kuhamishiwa Hospitali ya Nairobi ambako alilazwa hadi Januari 6 alipohamishiwa Ubelgiji anakoendelea na matibabu hasa mazoezi ya viungo.

Katika ujumbe wake alioutoa jana, Zitto ambaye yupo Ubelgiji kwa ziara ya kikazi, alisema alikutana na Lissu mwishoni mwa wiki iliyopita na kujadiliana kwa upana kuhusu masuala ya demokrasia.

“Lissu anasikitika kuwa Bunge mpaka leo sio tu halimhudumii, lakini pia hata stahiki zake za msingi kama mbunge hapewi,” alisema Zitto.

“Licha ya kutibiwa kwa misaada ya wasamaria wema, lakini ana mahitaji mengine kama mwanadamu na wajibu kama mzazi. Sheria ya Bunge imeweka wazi kuwa mbunge anapokuwa ametibiwa nje ya nchi Bunge humgharamia.”

Januari 30, kaka wa Lissu, Alute Mughwai alizungumza na wanahabari na kuhoji kitendo cha Bunge kushindwa kutoa stahiki za ndugu yake tangu aliposhambuliwa kwa risasi akisema ingawa anaendelea vizuri, lakini hajapata fedha zake za kujikimu na matibabu kama ambavyo sheria za Bunge zinaeleza.

Baada ya madai hayo, siku hiyohiyo Katibu wa Bunge, Stephen Kigaigai alilieleza Mwananchi kuwa Bunge linaendelea na mazungumzo na familia ya mbunge huyo kuhusu kumlipa stahiki hizo.

Katika maelezo yake, Zitto alisema licha ya Lissu ambaye pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kuhudumiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk Mpoki Ulisubisya alipokuwa katika Hospitali ya Dodoma mara tu baada ya kupigwa risasi, bado Bunge linasema linasubiri urasimu wa wizara hiyo wakati ni haki yake ya kisheria.

“Inasikitisha sana. Mzunguko ambao unafanywa na Bunge kuhusu suala lililo wazi kabisa la kugharamia maisha ya mbunge aliye kwenye matibabu linatia simanzi sana,” alisema na kushauri, “Ninamsihi Spika wa Bunge, achukue hatua kwenye jambo hili. Bunge litimize wajibu wake kwa mbunge wake kwa mujibu wa sheria. Kuendelea kuvuta miguu katika suala hili kunaleta hisia mbaya na kunajenga taswira mbaya ya Bunge letu.”

Mbali na suala hilo, Zitto pia aligusia uchunguzi wa shambulio la mbunge huyo na kuhoji sababu za kutoshughulikiwa mpaka sasa.

Alipoulizwa kuhusu mazungumzo hayo Lissu alisema, “Ni kweli nimekutana na Zitto na kuzungumza mengi ingawa yeye (Zitto) ameeleza kwa kifupi kuhusu mazungumzo yetu. Tumeongea mengi sana.”