Zitto alishukia Bunge matibabu ya Lissu

Muktasari:

Lissu yupo nchini Ubelgiji akipatiwa matibabu ya viungo na saikolojia.


Dar es Salaam. Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT Wazalendo),  Zitto Kabwe amemtembelea Tundu Lissu anayepatiwa matibabu katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha Leuven nchini Ubelgiji, kuhoji sababu za Bunge kutogharamia matibabu yake.

Mbunge huyo wa Singida Mashariki alishambuliwa kwa risasi zaidi ya 30, Septemba 7, 2017 na kupelekwa Hospitali ya Rufaa ya Dodoma na siku hiyo hiyo alihamishiwa Hospitali ya Nairobi ambako alilazwa hadi Januari 6 alipohamishiwa Ubelgiji anakoendelea na matibabu.

Katika ujumbe wake alioutoa leo Februari 12, 2018 Zitto ambaye yupo Ubelgiji kwa ziara ya kikazi, amesema alikutana na Lissu mwishoni mwa wiki iliyopita, kujadiliana kwa upana kuhusu masuala ya demokrasia.

“Lissu anasikitika kuwa Bunge mpaka leo sio tu halimhudumii lakini pia hata stahiki zake za msingi kama mbunge hapewi,” amesema Zitto.

“Licha ya kutibiwa kwa misaada ya wasamaria wema, lakini ana mahitaji mengine kama mwanadamu na wajibu kama mzazi. Sheria ya Bunge imeweka wazi kuwa mbunge anapokuwa ametibiwa nje ya nchi Bunge humgharamia maisha yake.”

Januari 30, 2018 kaka wa Lissu, Alute alizungumza na wanahabari na kuhoji kitendo cha Bunge kushindwa kutoa stahiki za ndugu yake tangu aliposhambuliwa kwa risasi, “ingawa Lissu anaendelea vizuri, lakini hatujapata fedha zake za kujikimu na matibabu kama ambavyo sheria za Bunge zinaeleza.”

Baada ya madai hayo, siku hiyohiyo Katibu wa Bunge, Stephen Kigaigai alilieleza Mwananchi kuwa Bunge linaendelea na mazungumzo na familia ya mbunge huyo kuhusu kumlipa stahiki hizo.

Katika maelezo yake Zitto amesema licha ya Lissu ambaye pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kuhudumiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk Mpoki Ulisubisya alipokuwa katika Hospitali ya Dodoma mara tu baada ya kupigwa risasi, bado Bunge linasema linasubiri wizara hiyo wakati ni haki yake ya kisheria.

“Inasikitisha sana. Mzunguko ambao unafanywa na Bunge kuhusu suala lililo wazi kabisa la kugharamia maisha ya mbunge aliye kwenye matibabu, inatia simanzi sana,” amesema,

“Ninamsihi Spika wa Bunge, achukue hatua kwenye jambo hili. Bunge litimize wajibu wake kwa mbunge wake kwa mujibu wa sheria. Kuendelea kuvuta miguu katika suala hili kunaleta hisia mbaya, na kunajenga taswira mbaya ya Bunge letu.”

Mbali na suala hilo, Zitto pia aligusia suala la uchunguzi wa shambulio lake akihoji sababu za kutoshughulikiwa mpaka sasa.

Lissu alipoulizwa kuhusu mazungumzo hayo amesema, “ Ni kweli nimekutana na Zitto na kuzungumza mengi ingawa yeye (Zitto) ameeleza kwa kifupi kuhusu mazungumzo yetu. Tumeongea mengi sana.”