Nabaki Afrika yalizwa na mauzo ya vifaa vya ujenzi wa nyumba kuporomoka

Mkuu wa Masoko wa Kampuni ya Nabaki Afrika, Princely Glorious (kulia) akitoa ufafanuzi wateja kuhusu bidhaa za kampuni hiyo walipotembelea katika banda la maonyesho ya kamapuni hiyo jijini Dar es Salaam. Picha na Salim Shao

Muktasari:

  • Hayo yamebainishwa na meneja mkuu wa Kampuni ya Nabaki Afrika, Mark McCluskey mwishoni mwa wiki iliyopita alipozungumza na gazeti hili kwenye maonyesho ya kimataifa ya utalii (Site).

 Kutokana na uchumi wa wananchi kubana, biashara ya vifaa vya ujenzi wa nyumba imepungua huku vile vya ukandarasi wa miradi mikubwa ikiongezeka zaidi ya mara dufu.

Hayo yamebainishwa na meneja mkuu wa Kampuni ya Nabaki Afrika, Mark McCluskey mwishoni mwa wiki iliyopita alipozungumza na gazeti hili kwenye maonyesho ya kimataifa ya utalii (Site).

Maonyesho hayo ya siku tatu yalimalizika mwishoni mwa wiki.

Tangu mwaka 2017 uanze, McCluskey alisema mauzo ya vifaa vya ujenzi yamepungua kwa asilimia 10 ikilinganishwa na ilivyokuwa mwaka jana.

“Tumeuza asilimia 50 ya vifaa hivyo mwaka huu. Hata hivyo, vifaa kwa ajili ya ujenzi wa barabara mauzo yake yameongezeka kwa asilimia 1,000 (mara 10 zaidi),” alisema McCluskey.

McCluskey alisema ongezeko katika mauzo ya vifaa vya utengenezaji wa barabara ni matokeo ya mipango na usimamizi wa Rais John Magufuli ambaye anatekeleza miradi mingi ya aina hiyo sanjari na kusimamia ubora.

Kuhusu kusambaza na kupigia debe bidhaa zinazotengenezwa nchini, McCluskey alisema kipaumbele chao kwenye bidhaa yoyote bila kujali ilikotengenezwa ni ubora.

“Kuna bidhaa kadhaa tunachukua nchini lakini nyingine tunaagiza kutoka nje ya nchi kupata ubora stahiki ambao unatufanya tuendelee kuwa imara sokoni,” alisema.

Aliongeza kuwa katika utengenezaji wa baadhi ya bidhaa inahitajika teknolojia ya hali ya juu ambayo wakati mwingine inakuwa bado haijafika nchini hivyo huwalazimu kuagiza nje ya nchi.

Siku kadhaa zilizopita ofisa masoko wa kampuni hiyo, Princely Glorious alisema wako kwenye mchakato wa kuingia ubia na kiwanda cha uzalishaji wa kemikali za ujenzi kilichopo Ujerumani kwa ajili ya kujenga kiwanda hicho hapa nchini.

Bila kutaja jina la kiwanda husika, Glorious alibainisha kuwa mchakato unaendelea vizuri na huenda ujenzi wa kiwanda hicho ambacho wamekuwa wakiuza bidhaa zake ukaanza kabla ya kuisha kwa mwaka huu.

“Kemikali hizo ni kama zile zinazozuia maji katika kuta. Baadhi ya taratibu zimekamilika tunatarajia bidhaa hizo ambazo huwa ni za ubora zitaanza kupatikana hapa nchini kwa wingi na bei nafuu,” alisema.