Taasisi ya kansa yanyoshea kidole chai, mirungi

Muktasari:

  • Kansa ya umio (eneo kati ya koo na mfuko wa chakula) inaongoza kwa vifo nchini Kenya ikifuatiwa na kansa ya mlango wa uzazi, matiti, utumbo na tezi dume kukiwa na vifo 4,354 kila mwaka.

Nairobi, Kenya. Kunywa chai ya moto wakati ukitafuna mirungi (miraa) na unywaji maziwa ya mgando (mursik) mara kwa mara imegundulika kuwa sababu inayoongoza watu kupata kansa ya umio au njia ya chakula Kaskazini mwa Kenya na Bonde la Ufa.
Taasisi ya Taifa ya Kansa ilisema Alhamisi kwamba takwimu zilizorekodiwa kutoka mikoa ya Bonde la Ufa, Mashariki Juu na Kaskazini Mashariki zinaonyesha idadi kubwa ya watu ambao wanasumbuliwa na kansa ya umio.
Kansa ya umio (eneo kati ya koo na mfuko wa chakula) inaongoza kwa vifo nchini Kenya ikifuatiwa na kansa ya mlango wa uzazi, matiti, utumbo na tezi dume kukiwa na vifo 4,354 kila mwaka.
"Sababu ya uwezekano wa hatari inayohusishwa na saratani ya umio katika uchunguzi uliofanywa huko Tenwek inaonyesha kuwa kinywaji cha moto na matumizi ya mursik yalikuwa yanahusishwa na kansa ya umio," alisema Alfred Karagu, kaimu mtendaji mkuu wa Taasisi ya Saratani ya Taifa.