Wafuasi wa Jubilee, Nasa kuonyeshana ubabe leo

Muktasari:

  • Raila Odinga amewataka wafuasi wake kujitokeza kwa wingi kwenye ofisi za IEBC
  • Lengo lao ni kwenda kumwondoa kwa nguvu Ofisa Mtendaji Mkuu wa tume hiyo
  • Jubilee nao wajipanga kwenda kumkingia kifua na kuzuia vurugu za aina yoyote

Nairobi, Kenya. Vyama viwili vyenye nguvu nchini vinatarajiwa kuonyeshana nguvu jijini Jubilee na muungano wa Nasa pale wafuasi wao watakapojimwaga mitaani kuandamana hadi kwenye ofisi za Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Kiongozi wa Nasa Raila Odinga alitoa wito jana kwa wafuasi wake kujitokeza kwa wingi katika maandamano kwenye makao makuu ya IEBC yaliyoko jengo la Anniversary Towers lengo likiwa kumtoa kwa nguvu Ofisa Mtendaji Mkuu wa IEBC Ezra Chiloba kwa madai ya kuhusika kuharibu uchaguzi mkuu uliofanyika Agosti 8.

Maandamano hayo yanafanyika siku chache baada ya Mahakama ya Juu kufuta ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta.

Hata hivyo, kikundi cha wafuasi wa chama tawala cha Jubilee kikiongozwa na mwenyekiti wa GEMA tawi la Nairobi, Wilfred Kamau, kimesema kitafanya maandamano ya kumkingia kifua Chiloba. Kikundi hicho kimepanga kufanya maandamano hayo hadi kwenye ofisi hizo zilizoko Anniversary Towers kumpa ulinzi ofisa huyo.

"Tunaahidi kwamba kadri wao wanavyojiandaa kwenda kumng’oa Chiloba, sisi tutakuwa pale kumlinda Chiloba lakini pia maslahi ya Wakenya,” alisema Kamau.

Mwenyekiti wa IEBC, Wafula Chebukati alikosoa msimamo wa Nasa wa kutoa vitisho dhidi ya tume yake akisema Mahakama ya Juu haikumtia hatiani ofisa yeyote wa IEBC kutokana na aibu ya uchaguzi huo.