Finca yawatangazia bingo wenye wazo bora la biashara

Muktasari:

  • Programu hiyo ni sehemu ya kusherehekea miaka 20 ya Finca nchini

Dar es Salaam. Benki ya Finca Microfinance imezindua programu ya kuwaongezea uwezo wajasiriamali wadogo kwa kuwapa stadi za biashara.

Pamoja na maarifa hayo, benki hiyo itatoa Sh10 milioni kwa wazo bora la biashara litakalowasilishwa na wajasiriamali hao.  

Mkuu wa idara ya masoko na mawasiliano wa benki hiyo, Nicholous John alisema programu hiyo ya miezi minne itafanyika kwa wateja wa jijini Dar es Salaam, kabla ya utaratibu wa kuipeleka mikoani.

Amesema mtu atakayekuwa na wazo bora zaidi atawezeshwa kifedha kuendeleza biashara ndogondogo.

"Shindano hili litashirikisha wateja wenye akaunti Finca na wanaopenda kushiriki watatakiwa kufungua kwa kuweka Sh20,000,” amesema.

Amesema washiriki watapaswa kujaza fomu zilizopo kwenye matawi wakibainisha watakachofanyia fedha watakazoshinda iwapo wataibuka  washindi. 

Miongoni mwa washiriki watakaojitokeza, amesema wanane watachaguliwa na jopo la majaji kushiriki katika kipindi cha runinga cha ‘kuza ofisi na Finca.’

“Mwishoni mwa shindano, mshindi mmoja ataondoka na zawadi nono ya zaidi ya Sh10 milioni," amesema.

Ofisa mkuu wa biashara wa benki hiyo, Emmanuel Mongella amesema programu hiyo ni sehemu ya kusherehekea miaka 20 ya Finca nchini.