Thursday, September 14, 2017

Jambazi ‘mstaafu’ aanika maisha yake, amshukuru IGP Sirro

Mwandishi wa gazeti hili mkoani Tanga, Raisa

Mwandishi wa gazeti hili mkoani Tanga, Raisa Said akizungumza na Nuni Dunduu katika soko la Mgandini jijini Tanga anapofanyia biashara. Picha na Maktaba 

By Raisa Said, Mwananchi rsaid@mwananchi.co.tz

Siyo rahisi kuamini kuwa mtu aliyekuwa jambazi kwa miaka mingi anaweza kuacha uhalifu huo na kujitokeza hadharani kueleza namna alivyokuwa akiendesha maisha yake.

Hata hivyo, hali ni tofauti kwa mkazi wa Tanga, Nuni Dunduu (50) ambaye alikuwa jambazi kwa takriban miaka 25, lakini miaka minane iliyopita alijitokeza hadharani na kutangaza ‘kustaafu’ kufanya vitendo hivyo.

Dunduu alichukua hatua hiyo mwaka 2009 wakati huo Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga alikuwa Simoni Sirro ambaye hivi sasa ni Inspekta Jenerali wa Polisi. Akionyesha kufurahishwa na kitendo hicho, Sirro alimpa Dunduu Sh50, 000 kwa ajili ya kuanzisha biashara.

Miaka minane imepita na Dunduu anayejiita Sirro Mdogo ana mengi ya kusimulia kuhusu maisha yake mapya na ya yale za zamani.

Akiwa ameketi na marafiki zake kwenye eneo lake la biashara ya kuuza mitumba lililopo katika soko la Mgandini jijini Tanga, Dunduu anasimulia baadhi ya mambo aliyokuwa akifanya.

Awali, mwandishi wa habari hii alikuwa na wasiwasi iwapo Dunduu angekubali kusimulia historia ya maisha yake, lakini alipata matumaini baada ya kuona akipokewa kwa furaha na mfanyabiashara huyo ambaye hivi sasa anatumia muda wake wa ziada kuwaasa vijana kuacha kujiingiza kwenye makundi ya uhalifu.

Alianza ujambazi mwaka gani?

Dunduu anaeleza kuwa mwaka 1984 ndipo alipoanza kujiingiza katika ujambazi. “Kipindi hicho nilikuwa nikiishi Tanga mjini mimi na familia yangu, akiwemo mzazi wangu mmoja ambaye ni mama yangu kwa kuwa baba yangu alifariki nikiwa mdogo sana,” anasema Dunduu.

Dunduu ambaye ni mlemavu wa miguu anasema kilichomfanya aingie kwenye ujambazi ni marafiki zake na makundi ya watu aliokuwa nao karibu wakati huo. Anasema rafiki zake walikuwa wakifanya kazi hiyo licha ya kuwa na umri mdogo.

“Pia niliingiwa na tamaa baada ya kuona marafiki zangu wakati huo wanakuwa na fedha na wanawake hivyo na mimi wakanishawishi mpaka nikajiingiza kwenye vitendo vya ujambazi,” anasema Dunduu.

Anasema alifanya ujambazi kuanzia mwaka 1984 mpaka 2009 alipoamua kuacha nao.

Kitu ambacho hawezi kukisahau

Kifo cha rafiki yake wa karibu ambaye walikuwa wote katika ujambazi ndilo tukio ambalo akilikumbuka linamuumiza. Rafiki yake huyo alifariki dunia mjini Moshi baada ya kupigwa risasi na mfanyabiashara waliyetaka kumuibia.

Anasema kuwa walimfukuzia mfanyabiashara huyo ambaye alikuwa akitokea Tanga kwenda Moshi, lakini hawakuweza kupata kitu chochote zaidi ya kifo cha rafiki yake.

Maeneo aliyofanya uhalifu

Anaeleza kuwa hakumbuki ameiba sehemu ngapi nchini, lakini anachokumbuka ameiba mali katika mikoa ya Tanga, Pwani, Morogoro, Dar es salaam na maeneo mengine ya nchi.

Anaeleza kuwa hawakuwa na muda maalumu wa kutekeleza uhalifu, bali walikuwa wanautumia muda wowote watakaoona unafaa baada ya kupewa taarifa na watu wa karibu na eneo wanalotaka kuiba, wakiwema walinzi wa maeneo husika.

Imani za kishirikina

Dunduu anasema kuwa majambazi wengi wanaamini imani za ushirikina hata yeye alikuwa akitumia hirizi wakati wa kwenda kuiba na kwamba dawa hizo alipewa na mganga wa jadi kutoka wilayani Muheza ambaye kwa sasa ni marehemu.

“Nilikuwa nikishika hirizi hiyo hata polisi walikuwa hawawezi kumuona na kumshika,” anasema.

Kitu gani kilimfanya aache ujambazi?

Anasema kilichomfanya aache ujambazi ni kutokana na kuchoka kuishi kwa wasiwasi kama mkimbizi kwa kuwa wakati wote hakuwa akimwamini mtu yeyote aliyekuwa akikutana naye.

“Nilikuwa nahisi kila mtu ambaye simfahamu ninayemwona ametumwa aje kunikamata,” anasema na kuongeza kuwa pia alitaka awe karibu na ndugu zake ambao walimtenga wakati anafanya ujambazi.

Sababu nyingine iliyomfanya aache ujambazi ni kutokana na marafiki zake wengi waliokuwa wakishirikiana nae kufariki dunia na wengine kufungwa jela kati yao vifungo vya maisha akiwamo mganga wa kienyeji aliyekuwa akimtegemea ‘kumlinda’ kimazingara.

Polisi wamtishia maisha

Anasema jambo la kushangaza ni kuwa baada ya kuacha rasmi ‘kazi’ hiyo mbaya alipata vitisho kutoka sehemu mbalimbali, lakini kilichomshtua zaidi ni kupata vitisho kutoka kwa baadhi ya askari wa jeshi la polisi mkoani Tanga.

“Askari wengi walionitisha ni wale ambao wanajihusisha na kazi hiyo ya ujambazi. Walikuwa wanahisi kuwa kwa sababu mimi nimeacha kazi hiyo nitawataja,” anasema Dunduu.

Hata hivyo, anasema kitu kikubwa anachojivunia ni Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Sirro kwasababu alipokuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, ndiye alimpa ulinzi ambao anao mpaka sasa.

Dunduu anasema kuwa anamshukuru sana mkuu huyo wa polisi kwa kuwa ndiye amemfanya aweze kuishi hivi sasa maisha mazuri na huru kama raia wengine wa Tanzania pamoja na kumwezesha kufanya biashara ambayo kwa sasa inampatia kipato.

Anajuta

Anasema kitu ambacho anakijutia ni kuingia kwenye ‘kazi’ hiyo ambayo mama yake mzazi aliyemtaja kwa jina moja la Joyce hakupendezwa nayo. Anasema kuwa jambo hilo lilimfanya atengwe na familia yote wakiwemo kaka zake, dada zake pamoja na ndugu na jamaa wa karibu na familia ya Dunduu.

Familia

Kwa sasa Dunduu anaishi na mke wake na tayari amefanikiwa kupata watoto wawili (wa kike na wa kiume). Anasema wa kiume anasoma darasa la nne mkoani Dodoma katika shule ya kanisa.

Anaeleza kuwa anafurahia kuwa na familia jambo ambalo awali hakuwa analiweza kwa sababu wakati akifanya ujambazi fedha zote alikuwa akizitumia kwenye starehe.

Marafiki wazungumza

Baadhi ya marafiki wa Dunduu wanasema kuwa zamani rafiki yao alikuwa ni mkorofi, lakini hivi sasa amekuwa mtu mwema na anahubiri amani.

“’Tulimtenga Sirro Mdogo kipindi chote cha ujambazi, lakini baada ya kuacha tumekuwa tukishirikiana katika shughuli mbalimbali,’’ anasema mmoja wa marafiki zake.

Dunduu amemuomba Rais John Magufuli amsaidie mtaji kwasababu kwasasa ameyumba kutokana na baadhi ya bidhaa zake kusombwa na maji wakati wa mvua kubwa zilizonyesha jijini Tanga.

Kauli ya Sirro

IGP Sirro athibitisha kumpokea ofisini kwake mwananchi huyo ambaye alikuwa jambazi sugu na kusema kwa sasa wamekuwa marafiki wazuri na anahakikisha kuwa Dunduu si yule wa zamani kwa sababu amekuwa mtiifu na mzalendo kwa nchi yake.

IGP Sirro anawataka majambazi wengine ambao bado wanaendelea na kazi hiyo waache kazi hiyo mara moja na kujisalimisha kama alivyofanya Dunduu.

-->