Mwisho wa migogoro ya ardhi wakaribia

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi akipokea malalamiko ya kudhulumiwa ardhi kutoka kwa mkazi wa wilayani Mvomero, mkoani Morogoro.

Muktasari:

NUKUU

“Shabaha kuu ya ILMIS ni kujenga mfumo halisi, wenye kubeba taarifa zote za ardhi sehemu moja ili kuongeza usalama wa taarifa hizo na imani ya wananchi hivyo kuongeza huduma kwao.”
Dk Moses Kusiluka

Matumizi ya ardhi ni mabadiliko yanayofanywa na binadamu kwa mazingira ya asili au jangwani kulingana na mahitaji, lakini lengo ni kuwa na mazingira yaliyojengwa kama mashamba, malisho na makazi.

Hata hivyo, inaelezwa matumizi ya ardhi na usimamizi wake wakati mwingine huwa na athari kubwa kwa mazingira kwa maana ya maliasili, vyanzo vya maji, udongo, virutubishi, mimea na wanyama.

Kwa mfano, vyanzo vya maji katika eneo lililokatwa miti ovyo au kwenye mmomonyoko, itakuwa na tofauti ya ubora kuliko yale ya maeneo yenye miti mikubwa na misitu ya kutosha.

Kulingana na ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula  Duniani (FAO),  uharibifu wa ardhi umeongezeka kwa kiwango kikubwa karibu katika nchi nyingi duniani.

Tatizo hilo linadaiwa kusababishwa na  kukosekana kwa mipango muhimu  ya matumizi bora ya ardhi.

Tanzania yachukua hatua

Hata hivyo, baada ya Tanzania kulibaini hilo, tayari Serikali imeanzisha Mfumo Unganishi wa Taarifa za Ardhi, Kiingereza maarufu kwa jina la ‘ Integrated Land Management Information System (ILMIS), utakaosaidia kutoa taarifa muhimu za ardhi kwa wananchi.

Akizungumza hivi karibuni, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, alisema mradi huo unatekelezwa na wizara yake.

Anasema ILMIS inalenga kuboresha usalama na kiwango cha kuaminika cha shughuli za ardhi kwa kuanzisha mfumo wa taarifa za ardhi.

Lukuvi anasema mradi huo ni salama na unaoaminika, kwani utawezesha kutoa huduma za ardhi zenye gharama nafuu na zenye kuleta imani zaidi kwa wananchi kutokana na ulivyoundwa.

Akizungumza wakati wa warsha ya mafunzo ya uboreshaji utendaji wa wadau wa ILMIS iliyofanyika hivi karibuni katika Hoteli ya New Africa, Dar es Salaam, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Moses Kusiluka alisema changamoto katika sekta ya ardhi zinaikabili Tanzania kwa kadiri kumbukumbu za binadamu zinavyoweza kurudi nyuma.

Anasema tayari majaribio kadhaa yameshafanywa miaka michache iliyopita kwa lengo la kukabiliana na changamoto hizo.

Dk Kusiluka anasema katika muongo mmoja uliopita, kumekuwapo na majaribio kadhaa ya Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, kuweka taarifa na rekodi za ardhi katika mfumo wa kompyuta.

Akitoa mifano ya majaribio hayo ya Serikali kutafuta majawabu ya changamoto za ardhi, Naibu Katibu Mkuu alisisitiza:

“Huko nyuma, Serikali ilibuni na kutekeleza miradi ya Mfumo wa Taarifa za Ulipaji Kodi za Ardhi (LRMS), Mfumo wa Menejimenti ya Taarifa za Ardhi (Molis) na Mfumo wa Kusajili Maeneo ya Ardhi Yaliyopimwa (SRS), kwa kutaja machache tu. Lakini katika majaribio hayo yote kila mfumo ulikuwa unajitegemea na kusimama peke yake bila kuunganika ama kuwasiliana na mwingine.”

Dk Kusiluka anaongeza: “Hakuna shaka kuwa mifumo hii ilisaidia uwekaji taarifa na kuboresha mifumo ya kibiashara ya ardhi wizarani, lakini bado uunganishaji taarifa na uwezo wa kubadilishana taarifa hizo kwa wepesi ilibakia changamoto yetu kuu. Mifumo hiyo iliyokuwapo haikuweza kufanikiwa ipasavyo kutatua changamoto za jinsi ya kutunza, kuweka na kubadilisha taarifa za ardhi kwa urahisi na kwa wepesi.”

Hata hivyo, Juni 25 mwaka huu, kikosi kazi cha masuala ya matumizi ya ardhi kilichokuwa kimejumuisha wadau kutoka serikalini na asasi za kiraia, kilikutana na kukamilisha rasimu ya mkakati wa kukabiliana na changamoto za matumizi ya ardhi nchini.

Mkakati huo uliwasilishwa katika ngazi ya juu kwa utatekelezwa, kusimamiwa na kufuatiliwa.

Kwa mujibu wa Dk Stephen Nindi, aliyezungumza kwa niaba ya Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUP), Tanzania itakuwa miongoni mwa nchi zenye utulivu wa migogoro ya ardhi iwapo mpango huo utatekelezwa.

Mratibu wa programu ya ardhi wa shirika la kimataifa la Care, Mary Ndaro anasema maeneo mengi yakipimwa yatasaidia kuwapo kwa usalama wa miliki na hati miliki hususani kwa wananchi wa vijijini  ambao karibia asilimia 60 wanategemea ardhi kwa ajili ya kujipatia kipato.

Hivyo uamuzi unaochukuliwa sasa na Serikali wa  kuwekeza katika upangaji wa matumizi bora ya ardhi, utasaidia kupunguza kama siyo kumaliza kabisa migogoro ya ardhi nchini.

Wakati wadau hao wakizungumza hayo, Serikali inasema ili kutafuta jibu la pamoja la changamoto za namna ya kuweka taarifa za ardhi linalofanywa na Ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara ya Ardhi, imemwajiri mtaalamu ambaye atatekeleza kwa majaribio mpango wa kubuni, kuendeleza, kufunga na kuanza kutumia mfumo wa ILMIS, mradi unafadhiliwa na Benki ya Dunia (WB).

Mfumo huo unatekelezwa kwa majaribio katika Halmashauri za Kinondoni na Ubungo, mkoani Dar es Salaam.

Dk Kusiluka anasema ILMIS itaunganisha shughuli zote za menejimenti ya ardhi, usajili na uandikishaji wa shughuli zote.

“Mfumo huo pia utasaidia kazi ya kubadilisha rekodi za ardhi na ramani kutoka kwenye rekodi za makaratasi na kuzigeuza kuwa za kidigitali,” anasema.

Kwa mujibu wa Dk Kusiluka kazi hiyo iliyoanza Julai mwaka jana, itakamilika Julai mwaka 2018.

Anasema kipindi hicho kitafuatiwa na cha mwaka mmoja cha kuendelea kuangalia utendaji wa mfumo kabla ya kuanza kusambazwa nchi nzima.

 “Shabaha kuu ya ILMIS ni kujenga mfumo halisi, wenye kubeba taarifa zote za ardhi sehemu moja ili kuongeza usalama wa taarifa hizo na imani ya wananchi hivyo kuongeza huduma kwao,” anasema.

Nini kifanyike ili kukamilisha mpango huo?

Ili kufanikisha shabaha hiyo, hatua kadhaa zitachukuliwa wakati wa utekelezaji wa awamu kwa awamu.

Hatua hizo zitakuwa ni kubuni majawabu ya changamoto za ardhi ambazo zitawezesha kuboreshwa kwa huduma zote za ardhi kwa kuchukua hatua za kitaalamu, kusudi kuleta utulivu na usalama katika mfumo wa utoaji huduma za ardhi.

ILMIS itahakikisha inabadilisha mfumo wa kazi kutoka kwenye mfumo wa kutumia makaratasi na mafaili na kuweka kidigitali ili kurahisisha upatikanaji wa kwa kutumia kompyuta. 

Hata hivyo, inaelezwa ujenzi wa mfumo huo utakapokamili na kuanza kufanya kazi kwa ukamilifu, muda wa kuhakiki na  kuboresha taarifa za ardhi na hata kuhamisha miliki ya ardhi utafupishwa kuliko ilivyo sasa.

Dk Kusiluka anasema ILMIS utasaidia kulinda ardhi ya umma kwa kuzuia uvamizi wa maeneo tengefu, misitu, hifadhi ya barabara na ardhi nyingine ya umma.

Uvamizi wa ardhi ya umma, imekuwa changamoto kubwa nchini. Hivyo, ILMIS itaongeza uendeshaji na ulinzi wa ardhi ya maeneo ya hifadhi na maliasili.

Pengine kubwa zaidi kwa wananchi ni kwamba, ILMIS itawasaida kupunguza kero za rushwa zinazohusishwa na uhakiki, usajili na uandikishaji na uhamishaji wa miliki ya ardhi, anasema Dk Kusiluka.

Tatizo la rushwa

Kama liko jambo moja ambalo pengine kila Mtanzania anayemiliki ardhi nchini amekumbana nalo katika kuweka kumbukumbu zake za miliki ya ardhi ni rushwa.

Lakini Dk Kusiluka anasema ILMIS itaongeza uwezo wa Serikali na Taifa  kupambana na kero ya rushwa katika shughuli za ardhi.

Ni dhahiri kuondoka kwa kero ya rushwa kutaiwezesha ILMIS kuleta manufaa mengine kwa umma ambayo ni ongezeko la imani ya wananchi katika mfumo wa uendeshaji wa shughuli za ardhi, jambo ambalo kwa sasa halipo kwa sababu ya wingi wa changamoto katika uendeshaji wa shughuli za ardhi nchini. 

Kusiluka anaongeza pia kuwa ILMIS itaongeza uhusiano na mawasiliano kwa kuambatanisha wamiliki wa mali kwenye mali zao, na mali zenyewe.

Mpango huo pia utawasiliana moja kwa moja na kutoa taarifa za miliki na menejimenti ya shughuli za ardhi kwa njia ya kielektroniki kwa taasisi nyingine zitakazoteuliwa, zikiwamo benki, taasisi za kutoza kodi, kampuni na taasisi zinazofanya biashara ya kujenga, kuuza na kununua nyumba.