Simon Sirro: Huyu ndiye IGP aliyetamani kuwa Padri

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP),Simon Sirro akila kiapo katika sherehe zilizofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam jana.

Muktasari:

Nakumbuka katika mahojiano hayo ambayo niliambatana na waandishi wenzangu wa MCL pamoja na mambo mengine, Kamanda Sirro alituambia laiti isingelikuwa baba yake leo hii yeye angekuwa Padri.

Dar es Salaam. Ilikuwa Juni, mwaka 2016 siku niliyopata fursa ya kufanya mahojiano maalumu na aliyekuwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Simon Sirro.

Nakumbuka katika mahojiano hayo ambayo niliambatana na waandishi wenzangu wa MCL pamoja na mambo mengine, Kamanda Sirro alituambia laiti isingelikuwa baba yake leo hii yeye angekuwa Padri.

Kamanda Sirro alisema ndoto yake kubwa ilikuwa kuwa Padri wa Kanisa Katoliki kabla ya kukatishwa na wazazi wake na kuamua kujiunga na jeshi hilo nchini.

Alisema kama kuna jambo ambalo anaweza kujutia katika maisha yake ni hilo tu la kutokuwa Padri na kwamba alikuwa amefika katika hatua ya juu ambayo hata hivyo hakutaka kuiweka wazi.

Sirro ni kamanda wa tatu wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, aliteuliwa na Rais John Magufuli Februari 15, 2016 kushika wadhifa huo baada ya aliyekuwa kamanda wa kanda hiyo kuanzia mwaka 2008, Suleiman Kova kustaafu. Kabla ya Kova kamanda wa kanda hiyo alikuwa Alfred Tibaigana.

Akizungumza katika mahojiano hayo ofisini kwake, Sirro alisema: “Unajua kama Mungu ameniweka hai na kunipa kazi sina cha kujutia. Wakati nikiwa kijana nilikulia katika maadili mazuri na kusoma seminari, sikuwa na mambo mengi sana labda najutia kutokuwa Padri maana nilikuwa nimefikia hatua ya mbali sana.”

Kamanda Sirro ambaye ana sifa ya kuhamishiwa katika mikoa yenye matukio makubwa ya uhalifu na ujambazi, alipoulizwa sababu za kuacha upadri na kujiunga na Jeshi la Polisi alisema: “Ilikuja tu nikajikuta nimebadilisha mawazo, lakini kikubwa ilikuwa wazazi. Unajua wazazi kule kwetu Musoma ilikuwa hawakuelewi usipooa.”

“Mzazi aliona mimi ni kijana mkubwa akasema haiwezekani. Nilifika katika ngazi ya juu sana na siwezi kuwaambia maana hamuwezi hata kuelewa.” alisisitiza Sirro katika mahojiano hayo.

Aliwezaje kubadilika?

Katika mahojiano hayo Kamanda Sirro ambaye amewahi kuwa Kamanda wa polisi katika mikoa ya Tanga, Shinyanga na Mwanza alieleza jinsi alivyoweza kubadilika kutoka katika mtizamo na maadili ya kujiandaa kuwa Padri hadi kuingia kwenye upolisi.

“Fikiria zile amri kuu za Mungu. Kama unakuwa Padri si ndiyo unasimamia hizo. Unaniuliza niliwezaje kubadilika sasa kama ukiwa Padri mtu akivunja amri hizo unamfanyaje?” Alihoji Sirro ambaye alieleza kuwa anapenda zaidi kusikiliza nyimbo za kanisa hilo.

“Lazima mtu uendane na wakati na mazingira yaliyopo. Ningekuwa Padri mngekuja kunitembelea na kukuta chumba changu kina misalaba na pengine mngeshindwa hata kunihoji.”

Baadhi ya viongozi waliowahi kushika nafasi za juu serikalini na wakati huohuo ni viongozi wa kanisa au mapadri ni aliyekuwa Jaji Mkuu, Augustino Ramadhani.

Mwaka 2013 Jaji Ramadhan alisimikwa kuwa mchungaji wa Anglikana, Zanzibar. Amewahi kuwa Jaji Mkuu Zanzibar, Brigedia Jenerali wa JWTZ, Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania na Mahakama ya Afrika Mashariki. Mara nyingi amekaririwa akisema kazi za sheria hazitofautiani na za kiroho kwa vile zote zinahitaji utende haki.

Mapambano dhidi uhalifu ndiyo yamesababisha kuteulewa IGP?

Pengine swali hili linaweza kuwa gumu kwa wananchi au hata yeye mwenyewe kulijibu kwa kuwa anayefahamu kwa nini anafaa kuwa IGP ni aliyemteua yaani Rais John Magufuli lakini kumekuwapo na minong’ono ikieleza kuwa huenda ushupavu wake wa kupambana na uhalifu ikiwamo matukio ya mauaji yanayoendelea katika maeneo ya Ikwiriri na Rufiji.

Wengine walienda mbali zaidi na kuhusisha na zoezi zima la mapambano dhidi ya dawa za kulevya lililosababisha watu kadhaa kushilikiwa kwa tuhuma za kujihusisha na biashara hiyo haramu wakiwamo wasanii, wanasiasa na wafanyabiashara.

Lakini, kwake Sirro yeye kana kwamba alijiwekea hazina ya utendaji wake kwani alionyesha juhudi kubwa katika mapambano dhidi ya uhalifu huku akichukua hatua pindi matukio ya mauaji au uporwaji wa silaha yanapotokea.

Katika mahojiano hayo, Kamanda Sirro alisema polisi kuporwa silaha ni aibu na kufafanua kuwa kitendo cha askari kunyang’anywa silaha na majambazi ni fedheha kwao na Jeshi la Polisi na kwamba madhara yake ni makubwa kwa jamii.

Katika mahojiano hayo Kamanda Sirro alisema tukio la uvamizi wa kituo cha polisi cha Stakishari jijini Dar es Salaam na silaha kuporwa lilikuwa fedheha kwa Jeshi la Polisi, lakini akabainisha kuwa halikuwa na viashiria vya ugaidi bali ujambazi.

Kamanda Sirro, ambaye wakati wa tukio hilo alikuwa Msaidizi wa Kamishna wa Polisi wa Kanda ya Dar es Salaam alitoa kauli hiyo wakati nchi ikiwa kwenye mapambano makali na watu wanaodhaniwa kuwa majambazi ambao walikuwa na silaha kali, kiasi cha kustahimili kupambana na polisi kwa zaidi ya saa 10.

Akijibu swali kuhusu matukio ya askari kunyang’anywa silaha yaliyotokea kwa wingi mwaka jana, Kamanda Sirro alisema: ‘‘Yalikuwa aibu kwa askari na Jeshi la Polisi kwa ujumla. Ni aibu kubwa,” alisema Kamanda Sirro.

“Fikiria wewe ni kiongozi, unapata habari kwamba askari amenyang’anywa silaha, itakuwaje. Ni aibu kubwa kwa Jeshi la Polisi. “Na kuna athari mbili za kunyang’anywa silaha. Kwanza silaha hiyo inaweza kutumika katika matukio ya uhalifu, lakini pili hujui itatumikaje. Inaweza kutumika kwenye vikundi hatari. Silaha za Jeshi la Polisi ni zile ambazo haziuzwi madukani.”

Alipoulizwa alijisikiaje wakati watu wasiofahamika walipovamia Kituo cha Polisi Stakishari kilichopo Ukonga wilayani Ilala Julai 13 mwaka jana, Kamanda Sirro alisisitiza ilikuwa fedheha kwa Jeshi la Polisi. “Unapokuwa kiongozi halafu silaha ikichukuliwa, huwa ni tatizo kwetu na lazima itakupa shida,” alisema mkuu huyo wa zamani wa operesheni za Jeshi la Polisi.

“Ila namshukuru Mungu hatujapata changamoto kubwa.”

Hata hivyo alisema wakati wa tukio alikuwa likizo. “Lakini niliitwa kazini kutokana na tukio hilo. Lakini tulibaini baadaye kuwa ulikuwa ni ujambazi.”

Tukio la Stakishari lilikuwa miongoni mwa matukio kadhaa ya uvamizi wa vituo vya polisi mwaka jana.

Kabla ya uvamizi wa Stakishari, majambazi walivamia na kukiteka Kituo cha Polisi cha Ikwiriri kilichopo tarafa ya Ikwiriri, wilayani Rufiji, mkoani Pwani na kuwaua askari wawili, kupora silaha saba na kisha kulipua bomu. Pia walivamia kituo kidogo cha polisi cha Mngeta mkoani Morogoro na kupora bunduki aina ya SMG na magazini moja yenye risasi 30.

Pia, majambazi walivamia kituo kidogo cha Mkamba mkoani Pwani na kusababisha kifo cha askari mmoja na mgambo. Pia, walipora silaha tatu aina ya shotgun tatu, SMG mbili na magazini 30 kila moja ambazo zilikuwa kwenye ghala la muda zikisubiri kupelekwa kwenye kituo kikubwa kwenye ghala kuu la silaha.

Pia, majambazi walivamia kituo kikuu cha polisi cha wilayani Bukombe mkoani Geita mwaka juzi ambako askari wawili waliuawa na kujeruhi wengine watatu.

Kamanda Sirro pia alijigamba kwamba tangu ateuliwe kuongoza Kanda ya Dar es Salaam, Jeshi la Polisi limepambana na watu takribani 100 waliokuwa wakilitikisa jiji kwa uhalifu na ujambazi na kufanikiwa kuwadhibiti.

Hata hivyo alisema kuwadhibiti watu hao hakuna maana kuwa polisi imemaliza kabisa matukio hayo, bali inaendelea kupambana kuhakikisha jiji linakuwa katika hali ya usalama wakati wote.

Sirro alisema watu hao 100 walikuwa wakipora raia waliokuwa wanatoka benki, kuvamia nyumba za watu na kupora na kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya.

Alisema kuwadhibiti watu hao hakuna maana kuwa polisi imemaliza kabisa matukio hayo, bali inaendelea kupambana kuhakikisha Jiji linakuwa katika hali ya usalama wakati wote, huku akieleza mambo saba yaliyofanyika kufanikisha mkakati wake huo.

“Wapo wanaotangulia mbele ya haki na hao ni wengi maana walipambana na polisi. Huwa nawauliza askari mtu mwenye bunduki unamkamataje? Stahiki yake tunajua sisi tulioajiriwa kwa kazi hii.”

Kamishna Sirro alisema bunduki zilizokuwa zikitumiwa na baadhi ya majambazi hao ni za kivita kama SMG, ambazo alisema zinapokamatwa wahusika hufikishwa mahakamani na mahakama hutoa amri silaha hizo kurejeshwa serikalini au kuteketezwa kama zitakuwa zimeharibika.

Mwandishi wa makala haya ni Mhariri wa miradi maalumu wa magazeti ya Mwananchi anapatikana kwa barua pepe: [email protected]