Tanzania ya viwanda inamhitaji mwanamke mkulima mdogo

Mama Shujaa wa Chakula kutoka mikoa mbalimbali nchini wakiwa na mabango walipokuwa wakiandamana kabla ya kuanza kwa kongamano la wakulima wadogo wadogo wanawake, lililofanyika Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro hivi karibuni. Picha na Hellen Nachilongo

Muktasari:

Hata hivyo, kilimo kimekuwa tegemezi kwa nchi nyingi zinazoendelea hasa Afrika ambako wananchi wake wengi hukitegemea kama uti wa mgongo.

Mvomero. Sekta ya kilimo ni muhimu kwenye kukuza uchumi wa nchi yoyote duniani, kwa Tanzania inategemewa na zaidi ya asilimia 70 kuendesha maisha yao.

Hata hivyo, kilimo kimekuwa tegemezi kwa nchi nyingi zinazoendelea hasa Afrika ambako wananchi wake wengi hukitegemea kama uti wa mgongo.

Akizungumza kwenye kongamano la wakulima hivi karibuni, mkuu wa Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro, Mohamed Utaly anasema kilimo ni sekta ambayo inategemewa kwa ajili ya uchumi kutokana na chakula kinachozalishwa kuuzwa nje na kuingiza fedha za kigeni.

Pia, Utaly anasema wakulima wadogo hasa wanawake ndiyo chachu ya maendeleo ya kilimo nchini. “Ni ukweli usiopingika kuwa wanawake ndiyo wengi shambani kuendeleza kilimo kwa ajili ya chakula na biashara,” anasema Utaly na kuongeza:

“Kuelekea uchumi wa viwanda, tuimarishe usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake vijijini.”

Shirika lisilo la Serikali la Oxfam Tanzania kupitia mradi wake wa Mama Shujaa wa Chakula, hivi karibuni liliandaa kongamano maalumu.

Kongamano hilo lilihudhuriwa na Mama Shujaa wa Chakula kutoka mikoa mbalimbali nchini, ikiwamo Tabora, Mwanza, Njombe, Tanga, Kilimanjaro, Simiyu, Dodoma, Rukwa, Kigoma, Mtwara, Mara, Dar es Salaam pamoja na Zanzibar.

Meneja Kampeni wa Mradi wa Mama Shujaa wa Chakula, Jovitha Mlay anasema madhumuni ya kongamano hilo ni kuwakutanisha wakulima wadogo wadogo wanawake ili kuelezea changamoto mbalimbali wanazopambana nazo.

Mlay anasema moja kati ya changamoto wanazopata wakulima hao ni bajeti finyu, hivyo Serikali haina budi kutenga fedha za kutosha hasa kwenye sekta muhimu kama kilimo.

Kila bajeti inavyopungua kwenye sekta ya kilimo ndivyo kilimo kinavyozidi kudidimia,” anasema Mlay.

Anasema kuelekea uchumi wa viwanda, mwanamke mkulima mdogo anastahili kuwezeshwa ili kuzalisha zaidi chakula na kuuza mazao yake kujiinua kiuchumi.

“Waathirika wakubwa kwenye hili ni wanawake, ifikie muda Serikali ijue umuhimu wa kutenga bajeti ya kutosha, wanawake wakulima waliopo vijijini ndiyo wategemewa wa familia zako, bajeti ikiwa nzuri kilimo kitakua na wanawake wakulima watazalisha vya kutosha,” anasema.

Anaongeza kuwa takriban asilimia 80 ya uzalishaji chakula nchini hufanywa na wakulima wadogo na asilimia 60 hadi 70 wakulima hao ni wanawake, hivyo hakuna budi kuwapa kipaumbele.

Akichangia kwenye kongamano hilo, Edna Kiogwe kutoka Jukwaa la Mama Shujaa wa Chakula anasema usawa wa kijinsia katika masuala ya kilimo ni jambo muhimu kwa kuwa wanawake ndio washika mpini wa maendeleo ya familia na nchi kwa ujumla.

Kiogwe anasema usawa wa kijinsia umekuwa changamoto hasa vijijini ambako bado kuna uelewa hasi miongoni mwa jamii, hivyo ni wajibu wa Serikali kutoa elimu na kujua kuwa mwanamke anahitaji kumilikishwa ardhi na kutoa uamuzi katika familia kwani yuko mbele kwenye kupambana na umaskini.

Anatoa mfano wa mradi wa Oxfarm wa Mama Shujaa wa Chakula, ambao umekuwa na manufaa kwa wanawake wengi vijijini kwa kushindanishwa kwenye kilimo na kuwezeshwa kuanzia elimu na hata mtaji.

Bajeti, umiliki ardhi

Baadhi ya wakulima wanasema licha ya changamoto ya bajeti finyu kwa Serikali kwenye kilimo, umilikishwaji ardhi wanawake ni tatizo nchini.

Mkazi wa Kilosa, Oroshorwa Anna ambaye pia ni Mama Shuja wa Chakula wilayani humo, anasema mwanamke anaweza kuwa katika ndoa lakini hawezi kumilikishwa ardhi na mwenza wake, hivyo inawawia vigumu kuendesha kilimo chenye tija.

Anna anasema Mkoa wa Morogoro una ardhi kubwa kwa ajili ya kilimo hivyo Serikali iingilie kati ili nao wamilikishwe au watengewe maeneo yao kwa ajili ya kilimo kwa kuwa wanajua umuhimu wake katika kuendesha maisha yao na taifa.

Pia, anasema kwamba changamoto nyingine ni mabadiliko ya tabianchi kwenye kaya yake ambayo imemkuta kutokana na kupoteza ng’ombe 43 kutokana na mafuriko yaliyotokea wilayani humo hivi karibu.

“Elimu zaidi inahitajika kwetu wakulima kwenye suala ta mabadiliko ya tabianchi hasa wanawake, kwani tunapoteza mali zetu na huwa zinaturudisha nyuma kimaendeleo,” anasema Anna.

Anasema taasisi za mikopo zinatakiwa kutoa mikopo yenye riba nafuu kwa wakulima wadogo, kwa sababu nyingi zimekuwa zinatoa mikopo kwa riba kubwa.

Anna anasema changamoto nyingine inayowakabili wakulima wa mkoa huo ni migogoro ya mipaka kati ya wakulima na wafugaji.

Anasema migogoro ya ardhi imekuwa changamoto kubwa hivyo kuwafanya wakulima hao kushindwa kuendelea, hivyo Serikali iingilie kati kutoa suluhisho la mipaka kati ya wakulima na wafugaji. Mmoja wa wakulima wadogo, Winfrida Mzeru anasema Serikali ifanye utafiti wa kutosha ili kubaini dawa za wadudu waharibifu wa mazao shambani.

Mzeru anasema kwamba ingawa Serikali inatoa ruzuku ya dawa kwa wakulima vijijini, lakini haziwafikii na mara nyingi huuziwa kwa bei ya juu.

Pia, anawataka wakulima wenzake kufanyia kazi elimu waliyoipata na kuifikisha kwenye vijiji na kaya zao hivyo kuwa na elimu endelevu ya kilimo.

Akijibu baadhi ya changamoto, Utaly anasema kwamba katika kukabiliana nazo hasa za wanawake na vijana, wilaya hiyo imetenga zaidi ya Sh130 milioni kutoka vyanzo vyake vya mapato.

Hata hivyo, Utaly anawaomba wakulima hao kuunda vikundi endelevu vyenye weledi kwa ajili ya kupata mikopo midogo ya kuendeleza kilimo.

Anasema elimu zaidi kuhusu kuzitambua fursa mbalimbali za kilimo na uanzishwaji viwanda inahitajika, kwa kuwa kumuelimisha mwanamke ni sawa na kuelimisha taifa.

“Wilaya kwa kushirikiana na Sido tuna mpango wa kuendesha mafunzo bure ya namna ya kuanzisha viwanda vidogo kwa wanawake wakulima ili kwenda sambamba na sera ya Tanzania ya viwanda,” anasema.

Utaly anasema viwanda vinahitaji maligafi ili kujiendesha, hivyo wakulima hao wadogo wadogo wanawake wapelekewe elimu ya kuzalisha mazao bora kwa ajili ya viwanda hivyo.

Anaongeza kwamba mikopo ndani ya vikundi itawawezesha wanawake kununua pembejeo kama mbegu bora, mbolea pamoja na dawa.

Kuhusu kunyanyaswa kwa wanawake katika umiliki ardhi, Utaly anasema kila mwanamke anahitaji kukataa kunyanyaswa yeye binafsi na kujenga heshima ndani ya familiya yake.

Anasema kwamba kwa kufanya hivyo watasaidia kuweka usawa wa kijinsia.