Uchambuzi wa mapato na matumizi bajeti ya 2018/19

Wananchi wakifuatilia mjadala wa bajeti redioni. Ni muhimu kwa kila mwananchi kufa-hamu kiasi cha fedha kilichotengwa ili afuatilie matumizi. Picha ya Maktaba.

Muktasari:

  • Kama ilivyo mipango na bajeti nyingine, kuna mambo mengi ya kujadili kuhusu mpango na bajeti pendekezwa kwa mwaka 2018/19.

Machi 13, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango aliwasilisha mapendekezo ya mpango wa maendeleo wa Taifa na ukomo wa bajeti ya Serikali kwa mwaka ujao wa fedha.

Kama ilivyo mipango na bajeti nyingine, kuna mambo mengi ya kujadili kuhusu mpango na bajeti pendekezwa kwa mwaka 2018/19.

Sera ya mapato

Kama ilivyo katika bajeti za miaka yote, sera za mapato kwa mwaka 2018/19 zitalenga kuongeza vyanzo vya ndani kwa ujumla hasa vya kikodi.

Hii itafanyika kwa njia mbalimbali zikiwemo kurahisisha ulipaji wa kodi kwa kutumia mifumo ya kielektroniki, kurasimisha sekta isiyo rasmi, kuboresha mazingira kiasi cha kuvutia uwekezaji na biashara, kusimamia mfumo wa ukusanyaji maduhuli kwa njia ya kieletroniki na kuimarisha uhusiano na washirika wa maendeleo wanaotoa misaada na mikopo.

Ni muhimu kuhakikisha sera inaongeza mapato ya ndani kutoka vyanzo vyaya kikodi na visivyo vya kodi. Ni muhimu bajeti igharamiwe kwa mapato ya ndani kwa kiasi kikubwa iwezekanavyo.

Hii husaidia kupunguza utegemezi kutoka nje ambako wakati mwingine huwa kunakuwa na masharti yasiyotekelezeka. Pamoja na mambo mengine, mikopo huongeza deni la Taifa na changamoto za ulipaji wake. Licha ya masharti, misaada huweza kutofika kwa wakati uliotegemewa.

Sera ya matumizi

Katika bajeti yoyote, haitoshi tu kuwa na sera nzuri ya mapato bila sera nzuri za kutumia mapato husika kwa afya kiuchumi. Waziri wa Fedha amesema mwaka 2018/19, Serikali itatekeleza sera kadhaa za matumizi kama ilivyo katika miaka yote iliyopita.

Hizi ni pamoja na kusimamia nidhamu ya matumizi ya fedha za umma kwa lengo la kupunguza yasiyo ya lazima, kuziba mianya ya uvujaji wa fedha, kudhibiti malimbikizo ya madai mapya na kuelekeza kiasi kikubwa cha fedha kwenye miradi ya maendeleo.

Kufikia azma hii, Serikali imepanga kufanya mambo kadhaa ambayo ni pamoja na kuwianisha matumizi na mapato halisi yatakayopatikana kila mwezi, ununuzi utakaozingatia thamani ya fedha na kuendelea kufanya uhakiki wa madai mbalimbali na kuyalipa yaliyohakikiwa pamoja na kuimarisha maandalizi na uchambuzi wa miradi.

Utafiti unaonyesha matumizi mazuri ya fedha za umma ni kati ya mambo muhimu yanayochangia utayari wa walipa kodi kulipa kodi kwa hiyari hivyo ni muhimu sera hizi zikatekelezwa kikamilifu.

Vyanzo vya mapato

Mwaka 2018/19 lengo ni kukusanya zaidi ya Sh32.47 trilioni kutoka vyanzo mbalimbali. Mapato ya ndani yanayojumuisha ya makusanyo ya halmashauri yanatarajiwa kuwa Sh20.89 trilioni sawa na asilimia 64 ya bajeti yote.

Bajeti hii itakuwa na utegemezi wa nje kwa asilimia 36, japokuwa inabidi, si afya kwa uchumi. Utegemezi katika bajeti unaweza kuwa ovu la lazima lisiloepukika haipendezi kiuchumi. Athari za utegemezi ni pamoja na kutopata tunachotaka kwa kiasi na muda tunaotaka. Nyingine ni masharti yatokanayo na utegemezi hasa kwa misaada.

Kati ya mapato hayo, kodi itachangia Sh18 trilioni sawa na asilimia 13.6 ya Pato la Taifa. Mapato yasiyo ya kodi yanatarajiwa kufika Sh2.15 trlioni na vyanzo vya halmashauri Sh735.6 bilioni.

Vyanzo vingine vya mapato ni misaada na mikopo yenye masharti nafuu ya Sh2.67 trilioni kutoka kwa washirika wa maendeleo ambazo ni sawa na asilimia nane ya bajeti yote.

Serikali pia inatarajia kukopa Sh5.79 trilioni kutoka soko la ndani. Ukopaji ni jambo la kawaida hata hivyo ukopaji kutoka katika soko la ndani la fedha huweza kuwa na changamoto kadhaa ikiwemo ya kuisukumiza pembeni sekta binafsi katika soko la fedha.

Kama masoko ya ndani hayana fedha za kutosha, wakopeshaji hushawishika kuikopesha zaidi Serikali kuliko sekta binafsi. Hii ni kwa sababu Serikali ina misuli imara zaidi ya kifedha na kisiasa. Inapotokea sekta binafsi inakosa mikopo, haitakuwa afya kwa uchumi unaotegemea kuendeshwa na sekta binafsi kupitia mikopo.

Vipaumbele

Bajeti zote huwa na pande kuu mbili za matumizi; ya kawaida na maendeleo. Kwa kawaida, nchi hutumia kiasi kikubwa cha bajeti katika shughuli za kawaida kuliko za maendeleo.

Kwa miaka ya nyuma, uwiano ulikuwa kati ya asilimia 20 hadi 25 kwa bajeti ya maendeleo na asilimia 80 hadi 75 kwa bajeti ya matumizi ya kawaida. Katika bajeti ya kwanza ya awamu ya tano, uwiano huu ulikuwa asilimia 40 kwa 60.

Mwaka 2018/19, Serikali inapanga kutumia Sh20.46 trilioni sawa na asilimia 63 kwa matumizi ya kawaida yanayojumuisha kulipa sehemu ya deni la Taifa, mishahara na matumizi mengineyo.

Matumizi ya maendeleo yatakuwa Sh12 trilioni sawa na asilimia 37 zitakazotumika kujenga miundombinu mbalimbali. Nchi hufaidika zaidi kiasi kikubwa cha fedha hii kikitumika kulipa wakandarasi na watoa huduma wengine wa ndani kuliko nje.

Hii ina maana kuwa ushiriki wa Watanzania utakavyokuwa mkubwa katika kutekeleza bajeti ndivyo fedha nyingi zitabaki na kuzunguka ndani na kuwaneemesha wananchi wengi zaidi.

Kuimarika kwa mzunguko wa fedha husaidia kuchochea shughuli za uchumi, kutengeneza ajira na kukuza uchumi kwa ujumla. Hata hivyo wakandarasi na watoa huduma wa ndani lazima wawe na ushindani wa kutoa bidhaa na huduma bora za umma katika kuitekeleza bajeti husika.