Uturuki anzisheni ofisi ya ubalozi Z’bar - Dk Shein

“Iwapo hilo litafanikiwa, litasaidia kuendeleza uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo katika sekta kadhaa ikiwamo biashara kati ya wananchi wa pande hizo mbili.”

Muktasari:

Dk Shein alisema hayo alipozungumza na Balozi wa Uturuki nchini Tanzania, Ali Davutaglu aliyefika Ikulu ya Zanzibar kwa ajili ya kujitambulisha.

Zanzibar. Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein ameutaka uongozi wa Uturuki kuanzisha ofisi ya ubalozi mdogo wa nchi hiyo visiwani hapa ili uhusiano uliopo kati ya pande hizo uzidi kuimarika.

Dk Shein alisema hayo alipozungumza na Balozi wa Uturuki nchini Tanzania, Ali Davutaglu aliyefika Ikulu ya Zanzibar kwa ajili ya kujitambulisha.

Alisema Uturuki ikitumia fursa ya kufungua ubalozi mdogo kama zilivyo nchi za China, India, Msumbiji na Misri ushirikiano kati ya nchini hizo katika masuala mbalimbali ya kimaendeleo yatafanyika kwa wepesi zaidi.

Alieleza kuwa uchumi wa Zanzibar unategemea sekta ya utalii, hivyo ni vyema ushirikiano ukaimarika zaidi kwa watalii wanaokwenda Antalya, Uturuki kufika Zanzibar pia.

Dk Shein alisema mji wa kitalii wa Antalya umebarikiwa kuwa na vivutio vingi sambamba na hali ya hewa nzuri, sifa zinazofanana na Zanzibar, hivyo ni vyema ukawapo ushirikiano katika kuwaleta watalii Zanzibar.

Hata hivyo, Dk Shein aliipongeza Serikali ya Uturuki chini ya uongozi wa Rais Recep Tayyip Erdogan kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha miradi ya maendeleo ikiwamo sekta ya elimu kwa kutoa nafasi za masomo kwa wanafunzi wa Zanzibar kusoma nchini humo.

Balozi wa Uturuki nchini Tanzania, Ali Davutaglu alimuhakikishia Dk Shein kuendeleza uhusiano na ushirikiano wake kati yake na Zanzibar na kuahidi kuendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali kuleta maendeleo.

Alisema kuwa Uturuki itaendelea kutoa ushirikiano wake kwa Zanzibar katika kuendeleza miradi ya maendeleo ikiwamo sekta ya elimu na utalii.