Wadau wajitokeza kumsaidia aliyeolewa na kaburi

Meneja wa Mradi wa Tokomeza Ukeketaji Serengeti, Godfrey Matumu wa pili kutoka kulia akiahidi kutoa ng’ombe wawili wa maziwa kwa familia ya Esther Itembe katika Kijiji cha Kyambahi wilayani hapa, mkoani Mara hivi karibuni. Wa kwanza kulia ni Emmanuel Wang’ete mtoto mkubwa wa Esther. Picha na Anthony Mayunga

Muktasari:

Esther, mwenye ulemavu wa mguu, aliolewa mwaka 1987 na Samwel Wang’ete kwa mahari ya ng’ombe 15. Lakini mwanamume huyo hakuwa mume wake kama zilivyo ndoa za kawaida. Badala yake Samwel alikuwa anawakilisha kaburi la marehemu Mniko Wang’ete ambalo Esther hakuwahi kuliona wala aliyezikwa humo hamfahamu.

Makala mbili mfululizo za gazeti hili kuhusu Esther Marwa (45) mkazi wa Kijiji cha Kyambahi wilayani Serengeti ‘aliyeolewa na kaburi’, zimewagusa wasomaji ambao wameahidi kumpa ng’ombe wawili wa maziwa.

Esther, mwenye ulemavu wa mguu, aliolewa mwaka 1987 na Samwel Wang’ete kwa mahari ya ng’ombe 15. Lakini mwanamume huyo hakuwa mume wake kama zilivyo ndoa za kawaida. Badala yake Samwel alikuwa anawakilisha kaburi la marehemu Mniko Wang’ete ambalo Esther hakuwahi kuliona wala aliyezikwa humo hamfahamu.

Sasa anaishi na wanae sita ambao wamekosa elimu kutokana na uwezo duni wa familia.

Lakini sasa wadau wamejitokeza kumfuta machozi wakati dunia ikiekeleza kuadhmisha siku ya mwanamke duniani, ambayo jamii hutafakari kuhusu ukatili dhidi ya wanawake kutokana na mila na desturi zinazotengeneza mfumo dume.

Mradi wa Tokomeza Ukeketaji Serengeti kutoka Amref Health Africa Tanzania inashirikiana na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), halmashauri na wadau wengine kwa ufadhili wa UN WOMEN kutekeleza mradi huo wa kutokomeza ukeketaji.

Ofisa mradi huo, Godfrey Matumu anasema mwanamke huyo anahitaji msaada.

       “Sisi tutatoa ng’ombe wawili wa maziwa ili waweze kumsaidia yeye na watoto wake kupata maziwa kama lishe pia fedha, maana anahitaji msaada mkubwa wa vitu na kisaokolojia, tunategemea Februari mwaka huu tutamkabidhi,”anasema.

Anasema familia hiyo inahitaji msaada mkubwa kwa kuwa watoto hawasomi na wataendelea kuwa mzigo kwa familia na jamii na kuomba wananchi kuepuka kuzaa watoto watakaoishi kwenye mazingira magumu kwa misingi ya mila na desturi.

“Jamii inatakiwa kutambua kuwa kuna tatizo kubwa Mkoa wa Mara linalosababishwa na mila na desturi, watoto wanazaliwa kisha wanatelekezwa, lazima kila mmoja atoke na kuelimisha wenye nafasi za kukemea wakemee bila kukoma,”anasema.

Ofisa Mradi wa Tokomeza Ukeketaji Serengeti, William Mtwazi anasema hayo ni matokeo ya kukumbatia mila zenye madhara ambazo zinaongeza mzigo kwa taifa na jamii.

“Aliyetoa mahari ya kaburi lioe hayupo hawa watoto wanapata shida sana,” anasema.

Anadai kuwa Serikali za Mitaa zinawajibika kulinda na kutetea masilahi ya mtoto ili kuhakikisha kuwa watoto wanalelewa katika mazingira stahiki na kwa mujibu wa maadili ya jamii na taifa letu na hilo ni hitaji mojawapo la Sheria ya Mtoto Namba 21 ya Mwaka 2009.

Mtwazi ambaye kitaaluma ni Mwanasheria anasema katika sheria ya mtoto zipo haki nyingi zinazohusu watoto.

“Hawa wanaotokana na makaburi wanakosa haki nyingi kisheria, haki ya kuishi na kuheshimiwa, kutokubaguliwa, kupata jina, utaifa na kuwafahamu wazazi wake, haki ya kutoa mawazo, haki ya kurithi,” anasema.

Pia, sheria hiyo inatoa wajibu kwa wazazi, jamii, Serikali za Mitaa kulinda haki za watoto, kulinda watoto walio katika mazingira hatarishi, kuhakikisha wazazi ama walezi wanatimiza wajibu wa kulea na kutunza watoto ikiwemo kuwaepusha na ajira mbaya.

Ashikwa na bumbuwazi

Katika hali ambayo hakutegemea Esther anashikwa na bumbuwazi kusikia ahadi ya ng’ombe wa maziwa.

“Kweli Mungu ni mkuu kilio changu kimewagusa watu na kuahidi msaada mkubwa namna hiyo, hata nilikoolewa hawakuwahi kutoa kwa ajili yangu na watoto ambao waliwataka kama wajukuu,” anasema.

Anamshukuru mwandishi na gazeti la Mwananchi kuweka wazi matatizo yake na wanawake wengine ili watu mbalimbali zikiwemo mamlaka za Serikali zitambue na kuchukua hatua dhidi ya ukatili huo.

Viongozi wa dini washangaa

Viongozi wa dini mbalimbali wanashangazwa na ndoa za makaburi kwa kuwa hazipo kwenye maandiko matakatifu. Zinakiuka misingi ya dini na haki za binadamu na zinatakiwa kukemewa ili kuondoa tatizo hilo.

Mmoja wa viongozi wa dini ya Kiislam wilayani Serengeti, Ustaadhi Mikidadi Iddy anasema katika kitabu cha dini Kuran hakuna sehemu iliyoandikwa kuhusu ndoa za makaburi.

“Dini haitambui ndoa za namna hiyo, hayo ni mambo ya mila na desturi ingawa wanayoyafanya wengine wanadini pia,” anasema.

Anasema viongozi wa dini zote wanatakiwa kushikamana kutoa elimu ili jamii iweze kuondokana na mambo ambayo yanayochangia kutweza utu wa mwanadamu na kufuru kwa mwenyezi Mungu, maana ameeleza katika vitabu vyake kuwa ndoa ni muunganiko wa mume na mwanamke.

“Ndoa hizi athari zake zinaonekana wazi kwa kuwa waathirika wakubwa ni mke anayeolewa pamoja na watoto wake, kama hatutashikamana na Serikali na makundi mengine kutoa elimu ikiwemo kupiga marufuku, athari zake kiuchumi zinazidi kuwa kubwa,”anabainisha.

Mchungaji wa Kanisa la Jeshi la Wokovu wilayani hapa, Samwel Nguti anasema kwa mujibu wa dini hakuna ndoa za namna hiyo.

“Mtazamo wa dini hauna uhusiano bali hayo ni mambo ya mila na desturi, tena ambazo zina madhara kwa makundi mbalimbali,” anabainisha.

Anasema Serikali haitakiwi kunyamazia ukiukwaji wa haki za binadamu huo kwa kivuli cha mila na desturi.

“Miongoni mwa mambo yanayotakiwa kupigwa marufuku ni ndoa za makaburi maana tumeshuhudia makundi ya watoto wakihangaika kwa kukosa wazazi halisi,” anasema.

Anasema ukimya wa watendaji wa Serikali unaligharimu Taifa kwa kuwa wanabeba mzigo mzito kuhudumia watoto na wanawake wanaotokana na ndoa hizo, pia ni aibu kwa nchi kwa kuwa baadhi ya mashirika yanapata ufadhili nje kwa ajili ya kutoa elimu za athari za ndoa kama hizo huku mamlaka za Serikali zikijiweka pembeni.

Watoto wanapouliza baba huzua balaa

Mchungaji Nguti anasema watoto wanapokuwa wakubwa hutaka kujua baba yao hasa wanapokuwa wanatambuliwa kwa jina tofauti na mtu wanayemwona anaishi na mama yao.

“Hapo familia nyingi zilizo kwenye ndoa za makaburi hutawanyika, maana inamuumiza sana mama yao kuwaambia baba ambaye hata yeye hamjui,” anabainisha.

Mchungaji huyo ambaye anatoka kabila linaloendekeza mila na desturi hizo anasema, kimsingi mwanamke anayeolewa ndoa ya kaburi kuna uwezekano mkubwa anakuwa hamfahamu huyo anadaiwa kuolewa naye (kaburi) hivyo wengi hukosa ujasiri wa kuwaeleza watoto ambao wana haki ya kujua wazazi wao.

Wengine hutoroka

Anasema baadhi ya wanawake wanapotambua kuwa wameolewa na makaburi hutoroka na wengine huacha watoto wakihangaika kwa kuwa ni ndoa za aibu katika jamii na hata wanapokuwa na wenzao hudharaulika.

Ameshasaidia watatu kutoka ndoa za makaburi

“Wanawake watatu ambao ni waumini wangu nimewanasua kwenye ndoa za aibu kama hizo, wapo ambao tumewatafutia ufundi wa ushonaji nguo ili waweze kujitegemea na kujitafutia kipato na huo ndio ukombozi wa kundi hilo kifkra na kiuchumi na watakuwa na uamzi wa kuolewa na amtakaye,” anasema.

Nini kifanyike?

Mchungaji na wadau wengine wanasema Serikali isiache masuala ya ukatili wa kijinsia kushughulikiwa na mashirika yasiyo ya kiserikali, bali ishughulikie kwa nguvu zote ili kujenga Taifa lenye ustawi la watu wanaoheshimu haki za binadamu.