Wakazi wa Kyela washangilia meli kushushwa Ziwa Nyasa

Muktasari:

  • Wananchi hao wakiongozwa na viongozi mbalimbali wa Serikali na taasisi binafsi kushuhudia tukio hilo ambalo ni la kihistoria, walionekana wakiruka ruka na kuimba nyimbo za Kinyakyusa kuonyesha furaha yao huku wengine wakisikika wakitamka: “Sasa ndoto ya nchi ya viwanda imetimia, neema kwa wana-Kyela imekuja, tutafanya biashara, ajira zitaongezeka.”
  • Meli hizi kila moja ina uwezo wa kubeba tani 1,000 za mizigo ni kati ya meli tatu zilizotengenezwa na kampuni hiyo ikiwamo ya abiria, zote gharama yake ni Sh20 bilioni.

Hivi karibuni, wakazi wa Kyela Mkoa wa Mbeya, walilipuka kwa kupiga mayowe na shangwe za furaha baada ya meli mbili za mizigo zilizotengenezwa na kampuni ya kizalendo ya Marine Transport Ltd ya jijini Mwanza, kushushwa Ziwa Nyasa, kwa majaribio ya awali baada ya kukamilika kwa asilimia 95.
Wananchi hao wakiongozwa na viongozi mbalimbali wa Serikali na taasisi binafsi kushuhudia tukio hilo ambalo ni la kihistoria, walionekana wakiruka ruka na kuimba nyimbo za Kinyakyusa kuonyesha furaha yao huku wengine wakisikika wakitamka: “Sasa ndoto ya nchi ya viwanda imetimia, neema kwa wana-Kyela imekuja, tutafanya biashara, ajira zitaongezeka.”
Meli hizi kila moja ina uwezo wa kubeba tani 1,000 za mizigo ni kati ya meli tatu zilizotengenezwa na kampuni hiyo ikiwamo ya abiria, zote gharama yake ni Sh20 bilioni. Kukamilika kwa meli hizo, kutafungua fursa ya kukuza na kuboresha shughuli za kiuchumi, kibiashara na kijamii katika ukanda wa Ziwa Nyasa hasa katika mikoa ya Mbeya, Njombe na Ruvuma. Pia itakuwa kiunganishi kikubwa kibiashara na nchi jirani za Malawi, Msumbiji, Jamhuri ya Kidemorasia ya Congo, Zambia na Afrika Kusini na kuongeza mapato kwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na kwa nchi.

Kaimu Mkuu wa Bandari Kuu ya Itungi, Kyela, Ajuaye Msese anasema endapo majaribio hayo yatafanikiwa na kukamilika salama kwa ajili ya utoaji huduma, itakuza uchumi kwa kiasi kikubwa kwani kuna wateja wengi wameonyesha utayari katika kutumia usafiri wa njia ya maji, mara vyombo hivyo vitakapokamilika,” anasema na kuongeza:

“Meli hizo za mizigo, kila moja ina uwezo wa kubeba tani 1,000 kwa wakati mmoja, tofauti na zilizopo sasa zinazobeba tani 720 za mizigo. Hivyo utaona ni kwa kiasi gani, kukamilika kwa meli hizi tutakuwa tumeleta mapinduzi makubwa katika sekta ya usafirishaji wa majini,” anasema Msese.

Msese anasema kukamilika kwa miradi hiyo kutatoa ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja na itakuwa kichocheo kizuri cha kufunguka kwa Ukanda wa Maendeleo wa Mtwara hivyo kuzifanya Bandari za Mtwara na Mbamba Bay kuhudumia soko la Malawi na hivyo kupunguza ushindani wa Bandari za Msumbiji kwa Bandari ya Dar es Salaam.

Anasema, “Unajua sisi TPA ni wasimamizi tu wa hizi meli lakini hatuna mizigo, watumiaji wake ni wananchi wenyewe, hivyo ni wakati wao sasa kuhakikisha wanatumia fursa ipasavyo ili kukuza uchumi na kuifanya Tanzania iwe nchi ya viwanda.”

Anasema wao TPA wakiwa ni wasimamizi wakuu wa bandari zote za Ukanda wa Ziwa Nyasa ambazo ni Itungi, (bandari kuu), Kiwira na Matema zilizopo Kyela, Ndumbi, Lundu, Mkili, Njambe, Liuli na Mbamba Bay zilizopo Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma na Lumbila, Ifungu, Nsisi, Makonde, Lupingu na Manda zilizopo Ludewa mkoani Njombe, wamejipanga vilivyo kuona zinafanya kazi kwa ufanisi na wananchi wa mikoa hiyo wanapiga hatua za maendeleo ya kiuchumi na kuongeza pato la taifa kutokana na ongezeko la fursa zitakazojitokeza.

Mbali na hilo, Msese anasema baada ya kukamilika na kuanza kutoa huduma ya usafiri wa majini, pia uundwaji wa meli moja ya abiria umeshaanza ambayo nayo itakapokamilika itatatua tatizo kubwa la usafiri wa abiria kwani itakuwa ikibeba abiria 200 na tani 200 za mizigo kwa wakati mmoja.

Msese anasema aina ya mizigo inayohudumiwa katika bandari za Ziwa Nyasa ni makaa ya mawe, mbolea, saruji, mbao, mihogo, mahindi, dagaa, bati na mizigo mingine mchanganyiko ambayo itasafirishwa ndani na nje ya nchi kwa usalama na uhakika zaidi.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Marine Transport Ltd, Mhandisi Saleh Songoro anasema zoezi la awali la ushushaji meli hizo limekuwa la mafanikio hivyo kitakachofuata sasa ni matengenezo madogo madogo pamoja na ukaguzi wa ubora wake kutoka mamlaka tofauti ikiwamo ukaguzi wa ubora wa meli wa kimataifa unaosimamiwa na Shirika la Kimataifa la Usimamizi wa Meli la Bureau Veritas na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra).

“Zoezi hili la awali limekuwa la mafanikio makubwa, sasa tunaendelea na majaribio ya vitu vingine kama vile paipu, matenki, rada na GPS na baadaye Sumatra wataendelea na ukaguzi wao. Tunaamini mwisho wa mwezi huu tutakuwa tumekamilisha na baada ya hapo tutazikabidhi kwa TPA,” anasema Songoro. Akizungumzia ubora wa meli hizo, Songoro anasema uundwaji wa meli hizo umezingatia ubora wa kimataifa na kabla ya kuzikabidhi kwa TPA kwanza watakaguliwa na Shirika la Kimataifa la Usimamizi wa Meli (Bureau Veritas) ambao baada ya kujiridhisha kwa kila kitu, watatoa cheti cha uthibitisho.

‘Ondoa hofu, sisi tunasimamiwa na Bereau Veritas kwa ukaguzi, sasa hivi baada ya kukamilika watakuja kwa ajili ya ukaguzi wa mwisho na kutupatia cheti cha ubora wa kimataifa, hivyo meli hizi zina ubora wa kimataifa,” anasema Songoro.

Kuhusu meli ya abiria, Songoro anasema tayari wameshaanza kuiunda lakini kazi hiyo itafanyika kwa ukamilifu baada ya kukamilisha vitu vyote kwa meli za mizigo hivyo bado hajajua itachukua muda gani.

Songoro anasema mradi huo pia umewezesha kuwekwa kwa chelezo ya kwanza katika Bandari ya Itungi, ambayo ni ya pekee ziwani humo kwa upande wa Tanzania.

Anasema chelezo hiyo ina faida nyingi kwa TPA na taifa kwani itakuwa ni ya kudumu na itatumika pia kwa matengezo ya meli za nchini na nchi jirani kama vile Malawi na Msumbiji.

“Hii chelezo itapunguza muda wa kukosekana kwa safari za meli pindi zinapokuwa kwenye matengenezo nchini Malawi. Mathalani, mwaka 2012 Meli ya Mv Songea ilikuwapo Malawi kwa zaidi ya miezi sita ikifanyiwa matengezo na kuathiri huduma za usafiri katika Ziwa Nyasa,” anasema Songoro.

Mkazi wa Kyela, Alex Mbipile ambaye alishuhudia zoezi la ushushaji meli ziwani, anasema sasa nchi ya viwanda na fursa za ajira kwa wananchi kupitia bandari za Itungi na Kiwira kwa upande wa Kyela na maeneo mengine inaanza kuonekana.

Anasema, “Hii ni hatua moja kubwa sana kwetu, sasa wananchi wa Kyela kazi kwetu, tunapaswa kujipanga kukabiliana na fursa zitakazotokana na usafirishaji wa meli hizi, hapa tuna kila sababu ya kuishukuru Serikali kutimiza ahadi yake ambayo kimsingi ilitolewa na Rais aliyetangulia Jakaya Kikwete.”

Mkazi mwingine aliyeshuhudia zoezi la meli hizo kushushwa majini, Richard Kilumbo, anasema hatua hiyo ya kushusha meli hizo majini kwa mafanikio ni ishara tosha kwamba uchumi wa mtu mmoja mmoja kwa wananchi wa Kyela na wa maeneo mengine ya Ziwa Nyasa unanukia kuwa mkubwa.

Anasema wanaamini kwamba vijana wao watapata ajira nyingi za bandarini, na akinamama watajiongezea kipato kwa kufanya biashara za kupika chakula. Kadhalika anasema kuwapo kwa meli hizo kutasaidia kuboresha huduma ya usafiri kutoka ziwani hadi Kyela mjini.

“Wananchi wa Kyela, ambao kimsingi ndio tuliopo jikoni kabisa na ziwa hili pamoja na bandari zote mbili za Kiwira na Itungi ndiyo wanufaika wa kwanza kabisa, najua hapa sasa akinamama watauza chakula kwa wingi, vijana tutapa ajira nyingi, kwa ujumla Mji wa Kyela utachangamka kibiashara tofauti na ulivyo sasa,” anasema Kilumbo.