Binadamu ‘akaribia’ Sayari ya Pluto

Moja ya vyombo vya uchunguzi wa anga kikianza safari.     

Muktasari:

Baada ya mafanikio makubwa ya kutuma chombo kwenye sayari ya Mars, wanasayansi sasa wanakaribia kufikia mafanikio mengine makubwa; kufanikisha safari ya New Horizons kwenye sayari ya Pluto.

Watafiti hao wamejitoa kwa robo ya maisha yao kufuatilia vifaa hivyo ambavyo vinatarajiwa kutoa matokeo mengine hivi karibuni.

Baada ya mafanikio makubwa ya kutuma chombo kwenye sayari ya Mars, wanasayansi sasa wanakaribia kufikia mafanikio mengine makubwa; kufanikisha safari ya New Horizons kwenye sayari ya Pluto.

Kama ilivyo kwa Rover ambayo imeshatua sayari ya Mars bila ya kuwa na binadamu ndani nyake lakini inatuma picha za ardhi ya sayari hiyo, New Horizon nayo haina mtu ndani yake na inatarajiwa kuanza kutuma picha za mazingira ya sayari ya Pluto kuanzia kesho.

Chombo kilichoundwa na Taasisi ya Utafiti wa Anga ya Marekani (Nasa), kimeshasafiri maili bilioni tatu na sasa kinakaribia mwisho wa safari yake ya miaka tisa kuelekea kwenye sayari ndogo ya Pluto.

Picha za kwanza zitatoa taarifa zaidi ya vidoa vya mwanga baada ya chombo hicho kufika anga ya Pluto. Kwa sasa New Horizons imebakiza maili milioni 100 kufika sayari ya Pluto.

Hata hivyo, picha hizo zilizopigwa kwenye sayari hiyo iliyojaa nyota, zitasaidia wanasayansi kupima umbali uliobakia na kuweka mikakati ya New Horizon kutua kwenye ardhi ya Pluto ifikapo mwezi Julai.

Ni safari ya kwanza kuandaliwa na binadamu kwenda Pluto, na wanasayansi wana hamu kubwa ya kuanza harakati za ugunduzi kwenye sayari hiyo.

“New Horizons imekuwa ni mradi uliochelewa kutokana na mambo kadhaa, lakini sasa mambo yanatokea,” alisema kiongozi wa mradi huo wa wanasayansi, Hal Weaver wa maabara ya fizikia ya Chuo Kikuu cha Johns Hopkins.

“Itakuwa ni mwendo wa kasi katika miezi saba iliyosalia, hasa kuelekea mwisho,” alisema Ijumaa iliyopita. “Tuna hamu kubwa ya kuifanya Pluto kuwa kwenye ulimwengu halisia, badala ya kuwa kitu kidogo, badala ya kuwa kitu kidogo cha kuchora.”

Chombo hicho kilirushwa Januari mwaka 2006, ikiwa ni mradi uliogharimu Dola 700 milioni za Marekani na katika siku za karibuni kilizinduka baada ya ya kipindi cha kulegalega kilichokuwa mapema mwezi uliopita.

Waongozaji vyombo vya angani walitumia wiki kadhaa zilizopita wakikiandaa chombo hicho kwa ajili ya kukamilisha safari yake, hasa kutua.

“Kwa baadhi yetu, wamekuwa wakishughulika na mradi huu kwa zaidi ya robo ya maisha yao kwenye fani, ili kufanikisha mpango huu,” alisema meneja wa mradi, Glen Fountain kutoka Applied Physics Lab. “Sasa tumekaribia kufikia mwisho.”

Kamera yenye uwezo wa kupiga picha kutoka mbali, itachukua picha za sayari ya Pluto katika miezi kadhaa ijayo.

Kifaa hicho kilituma picha katikati ya mwaka jana kabla ya kupumzika, lakini hizo zinatarajiwa kuonekana vizuri zaidi.

Wakati New Horizons ikisafiri kuelekea sayari ya Pluto, ilipiga picha za sayari hiyo ndogo ikionekana ya kuvutia pamoja na mwezi wake unaoitwa Charon.

Chombo hicho kilipiga picha hizo wakati kikiwa kwenye anga ya Pluto. Picha 12 ambazo zilitumiwa kuchora sayari hiyo, zilipigwa kutoka umbali wa kati ya maili milioni 267 na milioni 262 (sawa na kilomita milioni 429 na milioni 422).

Kwa kuziweka pamoja, picha hizo zinaonyesha sayari ya Pluto na mzunguko wake mzima kwenye mwezi huo unaoitwa Charon, ambao uko maili 11,200 (sawa na kilomita 18,000) kutoka ardhi ya sayari hiyo.

Mwezi wa Charon ni karibu nusu ya sayari ya Pluto. Mwezi huo ni mkubwa sana kiasi kwamba wakati mwingine huonekana kama sayari pacha na Pluto.

Timu hiyo ya wanasayansi sasa inatumia picha ambazo zinaionyesha Pluto kwenye mazingira yenye nyota na kupata eneo halisi ambalo New Horizons itapita kati ya Pluto na mwezi na nyota zake.

Setalaiti nne zilizoko Pluto ni ndogo sana kuweza kuonekana kwenye picha hizo za mbali, lakini zitaanza kuonekana kwenye picha za mwaka huu wakati New Horizon itakapoanza kutuma picha ikiwa karibu zaidi na Pluto.

Itakuwa siku chache kabla ya mpya kutumwa duniani, wanasayansi wanatarajia kuanza kuzionyesha mapema mwezi ujao.

Hadi kufikia Mei, picha za New Horizons zinatakiwa zifikie au kupita picha zilizopigwa na hadubini ya Hubble Space Telescope, na zinatakiwa ziwe bora kadiri siku zinavyokwenda.

Picha nzuri zaidi zitakuwa wakati New Horizons itakapokuwa juu ya Pluto Julai 14, umbali wa maili 7,700 na ikisafiri kwa mwendo wa kilomita 31,000 kwa saa.

Wanasayansi bado hawajajua sayari ya Pluto inaonekanaje nje ya Kuiper Belt.

Pluto ndiyo kitu kikubwa kwenye Kuiper Belt. Pamoja na mwezi wake wa Charon, ukubwa wa vitu hivyo viwili unaweza kufanana na ukubwa wa ardhi ya Marekani na bado sehemu fulani kubakia.

Applied Physics Lab ya mjini Laurel, Maryland nchini Marekani ilibuni chombo hicho cha New Horizons na kukitengeneza na sasa inaratibu safari hiyo iliyoandaliwa na Nasa.

Wakati New Horizons ilipoondoka duniani mwaka 2006, Pluto ilikuwa bado kwenye nafasi ya tisa katika mfumo wa jua.

Ilikuwa ni sayari pekee kwenye mfumo wa jua unaohusisha dunia ambayo ilikuwa haijafikiwa na vyombo vya anga vya duniani. Lakini miezi saba baadaye, taasisi ya unajimu ya kimataifa (International Astronomical Union) iliivua Pluto hadhi yake ya kuwa sayari ndogo, baadaye ikaitwa plutoid.