Tusiikamie sana Afcon 2019, tutafuzu siku ikifika

Muktasari:

Huku nyumbani, tumebaki kuwa watazamaji kama ambavyo tumetazama tangu tushiriki mara ya mwisho mwaka 1980, wakati huo likiitwa Kombe la Mataifa Huru Afrika.

Takriban juma moja limepita tangu kuanza kwa mashindano makubwa kabisa barani Afrika kwa ngazi ya Taifa, Kombe la Mataifa ya Afrika ambayo sasa yako katika hatua za fainali nchini Gabon.

Huku nyumbani, tumebaki kuwa watazamaji kama ambavyo tumetazama tangu tushiriki mara ya mwisho mwaka 1980, wakati huo likiitwa Kombe la Mataifa Huru Afrika.

Maswali na hoja za wadau ni lini timu yetu ya Taifa itapata nafasi ya kutuwakilisha kwenye michuano hii ya kikanda, ingawa nadhani swali linalofaa lingekuwa endapo tuna hadhi ya kucheza fainali za Afcon.

Kumbukumbu ya kufuzu mwaka 1980 nchini Nigeria bado ingali kichwani kwa wadau wengi wa soka, ikipimwa kama kilele cha mafanikio kwa soka yetu na kizazi kile.

Tusichojiuliza sana ni matokeo ambayo tuliyapata kwenye fainali zile na endapo tunaweza kujitutumua ikiwa tungefuzu tena miaka hii.

Stars ilitolewa katika hatua za awali kabisa michuano ya mwaka 1980, na ‘kizazi cha dhahabu’kinachohusishwa na na mafanikio yale hakijawahi tena kufuzu Afcon, si katika zama zao za kucheza, wala zama za ukocha na uongozi wa soka.

Tunaonekana kuyatukuza sana ’mafanikio’ ya 1980, katika namna inayopitiliza kiasi kwamba tunasahau kuwa miaka hii tuna sababu nyingi zaidi za kufuzu kuliko miaka hiyo, endapo tu hatutakuwa na haraka hiyo.

Kwa kuwa Taifa Stars haijafuzu kwa miaka mingi mashindano ya Afrika, hamu yetu imekuwa walau kushiriki tu kwa mara nyingine na wala sio kuwa miongoni mwa timu bora Afrika zinatakazoshindana hasa kwenye fainali hizo.

Mwanzoni mwa uongozi wa Rais Jakaya Kikwete, msisitizo wa kwanza kwenye soka ulikuwa ni kuunda timu ya taifa imara na kufuzu Afcon 2008, jaribio ambalo lilishindwa hata baada ya kuundwa kwa kamati ya kusaka ushindi iliyoongozwa na aliyekuwa mbunge wa Singida Mjini, Mohamed Dewji.

Licha ya juhudi zote za kiufundi na kisiasa, hatujafanikiwa bado kukata kiu yetu ya kushiriki Afcon na hadi sasa jinamizi lake linatuandama.

Ndiyo, linatuandama kwa kuwa imefika hatua ya wadau kurushiana maneno kuhusu uhalali wa msanii Diamond Platinumz kupewa bendera ya Taifa alipokuwa anakwenda kutumbuiza kwenye sherehe za ufunguzi za Afcon mwaka huu.

Hiki ni kichekesho kutoka pande zote, kwani sidhani kama Shakira hukabidhiwa bendera ya Colombia na Serikali yake kila mara anapoalikwa kutumbuiza kwenye Kombe la Dunia.

Wakosoaji nao wana haki ya kusema, kwani kwa kitendo hicho ni kama vile Serikali inajificha kwenye kivuli cha Diamond baada ya kushindwa kukata kiu ya washabiki ambayo ni kuwakilishwa na timu yao ya Taifa kwenye mashindano, na si msanii aliyejitengeneza mwenyewe.

Namna bora na kisasa ya kufuzu Afcon ni kwa kutengeneza timu imara, na si kwa mipango ya kisiasa inayolenga kukamia tu kufuzu mashindano ya Afrika au hata ya dunia.

Itazame Uganda kwa mfano, wao wamefanikiwa kumaliza kiu yao ya tangu 1978 ya kucheza Afcon lakini kila mdau wa soka anajua kuwa ile si kazi ya muda mfupi na ya kisiasa kama tunayojaribu kufanya sisi.

Kwa miaka kadhaa Uganda imepambana kuwa timu bora katika ukanda huu na safari yake Gabon ni ushahidi tosha.

Afcon ya mwaka 2019 nchini Cameroon imeshaanza kutazamwa kwa matamanio na Watanzania wa mlengo wenye kiu ya kufuzu tu, hasa baada ya kuona ratiba.

Bila shaka tunaweza kufuzu kwa ujanja ujanja wa kukamia mechi moja moja, tutafurahi kufuzu na kufuta aibu yetu ya miaka arobaini kasoro lakini tusitarajie matokeo tofauti na ya mwaka 1980, ukweli ni huo.

 

+255 713 049 852