Makosa katika Kiswahili, usahihi wake

Muktasari:

Katika makala ya leo nitaendelea kutoa ufafanuzi kwa makosa yaliyojitokeza na kueleza kwa ufasaha matumizi yaliyo sanifu.

Napenda kuchukua fursa hii kuwapongeza wasomaji wangu walioniletea maoni na mapendekezo kuhusu ufafanuzi ninaotoa wa matumizi fasaha ya Kiswahili.

Katika makala ya leo nitaendelea kutoa ufafanuzi kwa makosa yaliyojitokeza na kueleza kwa ufasaha matumizi yaliyo sanifu.

Katika magazeti niliyopitia nilisoma maandishi kama ifuatavyo: “ Kiasi hicho cha fedha kilitokana na mrahaba wa dhahabu Dola za Marekani.”

Waandishi wengi wanashindwa kutofautisha kati ya mrahaba na mrabaha. Sahihi ni mrabaha kwani ni faida au pato linalitokana na biashara. Maana nyingine ni malipo anayopewa mwandishi au msanii na kampuni iliyotoa kazi yake kila baada ya kipindi fulani cha mauzo.

“Mkazi mwingine Salum Hussein alisema ili kufikia malengo mazuri ya ukusanyaji wa fedha za michango.”

Huu ni mfano wa sentensi ambazo tunazisoma katika magazeti. Ilitarajiwa kuwa mwandishi angekamilisha mawazo yake, lakini hakufanya hivyo. Ameiacha sentensi ikining’inia hewani.

“Mkuu wa Jeshi la Polisi, Said Mwema akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu tukio lililotokea katika mkutano wa Chadema uliofanyika Soweto, Kata ya Kaloleni jijini Arusha jana.”

Kwanza ilitakiwa kueleza tukio lenyewe ni nini. Huu ulikuwa ni mlipuko wa bomu uliotokea katika mkutano wa Chadema.

Pili, mkutano huu ulifanyika katika Uwanja wa Soweto, Kata ya Kaloleni jijini Arusha.

“Kamanda huyo alisema mtuhumiwa atapandishwa mahakamani upelelezi ukikamilika.”

Kwa kawaida mtuhumiwa hupandishwa kizimbani baada ya kupelekwa mahakamani. Mahakamani kuna maeneo tofauti kwa kila mhusika. Kizimba ni ulingo ulio mahakamani uliojengwa kama sanduku ambamo mshtaki, mshatakiwa au shahidi husimama wakati wa kesi.

“ Hata hivyo vyombo vya usalama walifanikiwa kuwatoa mahabusu hao wakiwa wameumizwa.” Ni muhimu kuzingatia upatanishi wa kisarufi katika sentensi. Ni sahihi kuandika kuwa vyombo vya usalama vilifanikiwa … au wafanyakazi wa vyombo vya habari walifanikiwa…Kwa kuwa na ufahamu wa ngeli za Kiswahili makosa kama haya hayawezi kutokea.

“ Kuanzia Julai Mosi, kazi zote za wasanii ziwe na stika maalumu ili kupunguza uharamia. Neno uharamia halikutumika vizuri. Uharamia ni ujambazi wa kuiba na aghalabu hutokea baharini kwa kutumia nguvu. Uharamia huweza kuwa ni ugaidi au unyang’anyi wakati wizi ni neno la jumla la kuiba.

“Walifika katika hospitali hiyo ambapo wagonjwa wameumia vibaya.”

Tumezoea kusema kuwa fulani ameumia vibaya na tunalikubali, lakini siyo rahisi kupata kinyume cha kuumia vibaya. Kwa hiyo tunasema mtu ameumia sana au ameumia kidogo.

“ Wananchi wa Butiama, Mkoa wa Mara wanakabiliana na baa la njaa kali hali inayowapelekea kuishi kwa kutegemea kuokota makasha ya konokono ili wapate fedha za kununulia chakula.”

Kwa kawaida njaa haipelekei kuishi kwa kutegemea kuokota makasha ya konokono bali njaa inasababisha kuishi kwa shida na hivyo kuwafanya watu waokote magamba ya konokono. Pili, konokono hana makasha kwani makasha ni masanduku ya karatasi ngumu yanayotumika kuwekea nguo au vitu vya thamani. Neno sahihi ni koa. Koa maana yake ni gamba la konokono, pia huitwa kombe au chaza. Huweza kupatikana baharini kutokana na viumbe wa baharini wenye magamba.

“Vifaa vya ujenzi vilikuwa dhaifu.”

Vifaa vya ujenzi kama mchanga, matofali au hata sementi huweza kuwa chini ya viwango vilivyopendekezwa na hivyo kinachotengenezwa huwa hafifu na kuweza kusababisha matokeo mabaya. Kwa kutumia neno dhaifu tunapata maana ya kitu kilichodhoofu, konda, sinyaa au kufifia.

“ Mamlaka ya kodi duniani kote zinapaswa kubadilishana taarifa ili kuthibiti wakwepa kodi.”

Athari ya lugha ya asili inasababisha waandishi washindwe kutofautisha ya vitamkwa viwili ambavyo ni /dh/ na /th/. Lugha nyingi za asili hutufanya tushindwe kumudu Kiswahili sanifu na fasaha. Tatizo hili lipo na suluhu ni kuwasomesha walimu wetu katika taaluma ya isimu, hasa fonolojia.

Matokeo yake yatakuwa ni mafanikio makubwa katika kukamilisha lengo letu la kuwaandaa Watanzania wenye ujuzi wa lugha ya Kiswahili.