Benki ya Kilimo iwe chachu ya maendeleo ya mkulima

Yamekuwapo maneno mengi ya kumhamasisha mkulima kuongeza uzalishaji kuhakikisha dunia inakuwa na chakula cha kutosha kinachokidhi mahitaji.

Nchini, kilimo ndio uti wa mgongo wa Taifa. Takwimu za Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) mwaka 2016 zinaonyesha kilimo kinachangia asilimia 29.1 kwenye pato kuu la Taifa (GDP).

Bado kuna fursa kubwa katika kilimo hususan kwa wakulima wadogo ambao wengi wapo vijijini ingawa wanakosa uwezeshwaji wa mtaji.

Kwa kutambua umuhimu wa kilimo, Serikali ilianzisha Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) ili kuwanasua wananchi wengi kutoka katika lindi la umaskini kupitia kilimo chenye tija na manufaa kwa mkulima.

Natambua mambo mengi makubwa yaliyofanywa na benki hiyo kuwawezesha wakulima mbalimbali nchini ila bado zipo changamoto nyingi ili kuwafikia wakulima wadogo kama kweli tuna nia ya kupunguza umaskini kama sio kuumaliza kabisa.

Kufanikisha mambo hayo ni vyema TADB ikawageukia wakulima wadogo licha ya changamoto za kuwakopesha zilizopo. Hizi zisiwe sababu ya kuwaacha na kuwakopesha wafanyabiashara wa mazao yao. Wakulima hawa wakikopeshwa, tutafanikiwa kutekeleza malengo endelevu ya Umoja wa Mataifa ya kutokomeza njaa na umaskini.

Nitakueleza namna benki hiyo inavyoweza kuyafikia makundi mbalimbali ya kilimo hususan vijana ambao kwa siku za usoni wameonekana kutokuwa na mwamko mkubwa wa kwenda shambani hivyo kuongeza wimbi la vijana wanaokimbilia mjini kufanya biashara huku wakiacha ardhi yenye rutuba tele ikiota nyasi na vichaka badala ya mazao.

Ili kufanikisha maono ya kuwa na uchumi wa kati unaotegemea viwanda, kilimo kina nafasi kubwa kwani ndicho kitakachotoa malighafi zinazohitajika viwandani. Hapa kuna fursa nyingi kwa TADB.

Miongoni mwa yanayoweza kufanywa ni kuanzisha na kusimamia vikundi vya wakulima. Kuna haja kubwa ya kujifunza kutoka kwa benki za biashara zilizofanikiwa kukopesha vikundi vidogo.

Benki ya kilimo ione haja ya kuanzisha vikundi vya wakulima wa mazao mbalimbali na kuviwezesha na kuacha kuwakopesha wafanyabishara kwani benki za biashara zipo kwa ajili yao.

Kingine benki hii inaweza kufanya ni kushirikisha fursa zilizopo kwenye kilimo kupitia mitandao ya kijamii. Ni ukweli usiopingika kwamba ukitaka kumpata kijana wa kisasa kwa urahisi kabisa basi tumia mitandao ya kijamii.

Watanzania wengi hususan vijana wanatumia muda mwingi katika mitandao ya kijamii kusoma habari mbalimbali ambazo wachambuzi wa mambo wanadai kwa sehemu kubwa haziwasaidii kutatua matatizo yao.

Pengine vijana hawajashirikishwa kwa kina fursa mbalimbali za kilimo na mamlaka husika ndio maana hawajauona mvuto uliopo hivyo kutopenda kujihusisha nacho.

Vijana wanapatikana kwenye mitandao ya kijamii. Huko ndiko wanakoweza kuelezwa fursa zilizopo kwenye kilimo na wakaelewa. TADB iwafuate huko na kuwavuta kwenye sekta hii nyeti.

Kingine kinachoweza kufanywa ni kufadhili mafunzo ya wakulima wajasiriamali. Njia muhimu ya kumsaidia mkulima ni kumpa mafunzo ya kilimo chenye tija.

Hili laweza kufanywa kwa kuwatumia wataalamu mbalimbali na ikibidi, kuwapeleka na kuwafunza kwa vitendo kutoka kwa wakulima waliofanikiwa. Kwa kufanya hivyo, benki sio tu itakuwa imejenga picha nzuri kwa jamii bali itawapa maarifa ya kudumu wakulima wengi wanaolima kwa mazoea.

Benki hii pia inaweza kutoa mikopo yenye riba nafuu kwa wakulima ili kuwawezesha kufanikisha miradi yao na kukuza uzalishaji.

Alipokuwa anazindua sera ya Taifa ya huduma ndogo za fedha mjini Dodoma mwaka 2017, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan alisema benki zitoe mikopo yenye riba nafuu ili kuwapunguzia mzigo Watanzania maskini.

Kama nia Serikali ni kupunguza umaskini basi riba ya mikopo bado ni tatizo linalohitaji mkakati endelevu kulishughulikia. Benki ya kilimo inapaswa kulipa kipaumbele suala hili kuhakikisha wakulima wanakopesheka na kuimarisha kipato chao bila kuumia.

Fursa nyingine iliyopo ni kushilikiana na taasisi za Serikali zenye mipango ya kumkomboa mkulima. Wahenga walisema kidole kimoja hakivunji chawa, kwa kuwa nchi ni yetu na lengo ni kuondoa umaskini basi ni vyema TADB ikashirikiana na taasisi nyingine ili kuleta mapinduzi makubwa katika sekta ya kilimo .

Mwandishi ni mkufunzi Chuo Kikuu Ardhi. Kwa ushauri na maoni anapatikana kwa simu namba 0765 666 255.